Habari Mseto

Walimu waonywa dhidi ya kuuza sodo za serikali

July 24th, 2018 1 min read

VIONGOZI kutoka Kaunti ya Turkana, wameonya walimu wa shule za msingi na upili dhidi ya kuuza sodo zinazotolewa na serikali bila malipo kwa wasichana wa darasa la sita hadi kitato cha nne.

Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Turkana, Bi Joyce Emanikor, Mbunge wa Turkana ya Kati, John Lodepe, na Kamishna wa Kaunti, Seif Matata, walisems sodo hizo zilitolewa na serikali kuu kusaidia wasichana hasa wanaotoka katika familia masikini.

Kulingana nao, hatua hiyo ya serikali ilinuiwa kulinda hadhi ya wasichana na kuwawezesha kuendeleza masomo yao bila matatizo.

Bi Emanikor alisema ni sharti walimu wote wahakikishe kuwa sodo zinapofikishwa shuleni mwao, zote zinapeanwa kwa wasichana waliolengwa kwa kiwango kitakachowasaidia kwa muhula mzima.

“Tunataka kila kaunti ndogo na kila wadi ipate sodo za kutosha kwa wasichana wanaolengwa na hakuna sodo zinazofaa kuekwa katika afisi yoyote ya elimu wala stoo ya shule,” akasema.

Kwa upande wake, Bw Lodepe alisema kila msichana anafaa kupewa pakiti nne ambazo zitawasaidia kwa muhula mzima jinsi ilivyonuiwa.

Alisema wasichana wengi wamekuwa wakikosa kwenda shuleni na wengine kuacha shule kwa sababu ya aibu wanazopitia wanapokuwa kwa hedhi.

Bw Matata alitoa wito kwa machifu, manaibu wao na manaibu wa kamishna wa kaunti kuhakikisha hakuna sodo yenye chapa ya serikali itauzwa madukani.

“Tutachukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayepatikana akiuza sodo hizo. Ninaomba pia wazazi wa wasichana wawe huru kutoa habari kuhusu mwalimu yeyote atakayeuza sodo hizo ili hatua zichukuliwe dhidi yao haraka,” akasema.