Habari Mseto

Walimu waonywa dhidi ya makahaba

August 13th, 2018 1 min read

Na WINNIE ATIENO

WALIMU wakuu wa shule za msingi kote nchini wanaokusanyika jijini Mombasa wameonywa dhidi ya kuzurura na viruka njia waliokita kambi katika jiji hilo la kitalii kwa lengo la kuwapora pesa zao.

Zaidi ya walimu 10,000 wamekongamana katika ukumbi wa Sheikh Zayed kwa mkutano mkuu wa walimu wakuu wa shule za msingi kote nchini.

Mada ya warsha ya mwaka huu ni ‘Elimu na Ujuzi’. Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kufungua rasmi mkutano huo kesho (Jumanne) huku walimu hao wakimtarajia azungumzie maswala tata yanayowakabili.

Naibu kamishna wa Kisauni Kipchumba Rutto alisema makahaba hao wanaweza kutumia dawa za kuwazuzua walimu hao kabla ya kuwapora mali yao.

“Tunaomba walimu wasiende maeneo au hoteli ambazo watawekewa dawa maarufu iitwayo mchele kwenye vinywaji vyao,” akasema Bw Rutto.

Akihutubia waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Sheikh Zayed, Mombasa, Bw Rutto alisema usalama umedumishwa kuhakikisha walimu hao wakuu wanalindwa dhidi ya utovu wowote wa usalama.

“Lakini ninawasihi msiende kutembea maeneo hatari ambapo vimada hao wamekusanyika tayari kuwanyemelea. Tumehakikisha tunaimarisha trafiki barabara za Mombasa huku kamati ya usalama ikiwahakikishia usalama wa kutosha,” akasema Bw Rutto.

Majuzi baadhi ya walimu wakuu wa shule za upili nchini waliohudhuria kongamano lao la kila mwaka Mombasa waliporwa mali yao kwenye hoteli walizokodi.

Alisema baadhi ya walimu ambao watakuwa wakilala eneo la Mtwapa, Bamburi na Malindi watapewa ulinzi wa kutosha.

Aidha, mkuu huyo wa usalama aliwashauri walimu hao kutoka zaidi ya shule 24,000 za msingi watembee kwa vikundi.

“Na wale wanaobugia mvinyo pia wakunywe kwa kiwango. Wasihadaiwe na viruka njia ambao wanatarajia kuvuna kwa walimu wakidhania wana pesa nyingi sana.

Tutalinda walimu kwa kila hali, lakini watembee maeneo salama hususan Mtwapa na Mombasa,” akasema Bw Rutto. Aliwaonya dhidi ya kukodi majumba au hoteli zilizoko vitongoji duni.