Habari Mseto

Walimu watahudumu miaka 10 kabla ya kuajiriwa – TSC

September 4th, 2020 2 min read

NA KITAVI MUTUA

WALIMU wanaopewa kazi ya kandarasi na Tume ya TSC sasa watatumika kwa miaka 10 kabla ya kuajiriwa kikamilifu.

Hii ni kinyume na Sheria ya TSC ya 2012 ambayo inaeleza kuwa muda wa kuhudumu kabla ya kuajiriwa kazi ya kudumu na yenye pensheni utakuwa miezi sita.

“Mwalimu anayepewa kazi na TSC atawekwa chini ya uangalizi kwa muda usiozidi miezi sita kabla ya kupewa kazi ya kudumu na yenye pensheni,” kinasema Kifungu 61. (1) A cha Sheria ya TSC, 2012.

Lakini sasa TSC imewaambia walimu wanaoomba kazi kwenye shughuli inayoendelea kuwa watahudumu kwa kandarasi kwa miaka 10 mfululizo wakiwa chini ya uangalizi kabla ya kuajiriwa kazi ya kudumu na yenye pensheni.Tume hiyo imo katika harakati za kuajiri walimu 11,574 katika shule za msingi na sekondari.

“Mnafahamishwa kuwa ili kuajiriwa kazi ya kudumu na yenye pensheni, mtu atahitajika kuhudumu kwa miaka 10 mfululizo akiwa chini ya uangalizi,” inasema notisi kwa wanaotaka kazi ya ualimu wa TSC.

Hii ina maana kuwa walimu hao wataajiriwa kazi 2030, ambapo ikiwa wakati huu mmoja atakuwa na miaka 35, atapewa kazi ya pensheni akiwa na miaka 45.

Katika muda huo pia hatapandishwa cheo chochote.Muda wa uangalizi katika uajiri hutumika kama wa majaribio ya uwezo wa mfanyakazi kutekeleza majukumu yake, na ikiwa mwajiri ataridhika basi humpa kazi ya kudumu.

Muda huo kwa kawaida huwa wa kati ya mwezi mmoja na miezi sita.Kulingana na Sheria ya Uajiri Kifungu cha 42, muda wa uangalizi wa mfanyakazi haupaswi kupita mwaka mmoja.

“Muda wa uangalizi hautazidi miezi sita, lakini unaweza kuongezwa kwa kipindi kingine kisichozidi miezi sita kwa makubaliano na mfanyakazi.”Hii ina maana kuwa TSC imekiuka sheria za uajiri.Tayari Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) ametaja hatua hiyo ya TSC kuwa kinyume cha sheria na Kipengee cha 42 cha Katiba.

“Huwezi ukamwajiri mwalimu kisha umwambie atapewa ajira ya kudumu na pensheni baada ya miaka 10. Tutapinga hili mahakamani,” akasema Bw Sossion.

Lakini Afisa Mkuu wa TSC, Bi Nancy Macharia alitetea hatua yake akisema notisi hiyo ni tahadhari kwa walio na zaidi ya miaka 45.