Habari Mseto

Walimu wataka maeneo ya kunyonyesha

July 23rd, 2019 1 min read

Na NDUNGU GACHANE

KUNDI moja la walimu wanawake linaitaka Wizara ya Elimu kubuni maeneo maalum ambapo wanawake walio na watoto wataweza kuwanyonyesha watoto wao.

Kupitia Chama cha Walimu Wanawake (Kewota), walimu hao wanataka Bunge la Kitaifa kupitisha sheria ambayo itaifanya iwe lazima kwa taasisi zote za elimu kubuni maeneo hayo.

Kulingana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bi Benta Opande, mswada huo utahakikisha kuwa walimu hao wanaweka bidii kazini na kuwaondolea wasiwasi. Alisema kuwa hilo pia litaimarisha matokeo ya wanafunzi katika shule husika.

Akizungumza na Taifa Leo Jumanne, Bi Opande alisema kuwa kwa sasa, chama hicho kinafanya mazungumzo na wabunge wanawake katika Bunge la Kitaifa na Seneti kuandaa rasimu ya mswada huo, ambapo badaye utawasilishwa ili kujadiliwa.

“Tunataka sheria maalum kupitishwa kuwaruhusu walimu wanawake kuandamana na wajakazi wao shuleni ili kuwawezesha kunyonyesha wanao kwa ajili ya kuimarisha utendakazi wao bila matatizo yoyote,” akasema Bi Opande.

Alisema kuwa hatua ya walimu hao kuwaachia wajakazi wao maziwa kuwapa wanao huwa inawaathiri sana kiakili, hali ambayo huwazuia kuzingatia utendakazi wao kikamilifu.

Alisema kuwa hali hiyo pia si nzuri kiafya kwa watoto ambao wanapaswa kunyonyeshwa.

“Hatua hizo zimewekwa katika kampuni za kibinafsi na zimeimarisha sana matokeo ya kikazi miongoni mwa wanawake walioajiriwa. Hivyo ndivyo tunavyotaka katika shule zetu. Wanawake wamebaguliwa kwa muda mrefu na hiyo ndiyo sababu yetu kubuni chama hiki ili kutetea maslahi yao,” akaongeza Bi Opande.