Habari Mseto

Walimu wataka shule zifungwe Covid ikisambaa

November 2nd, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

WALIMU nchini, sasa wanataka serikali ifunge shule kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona.

Maafisa wa vyama vya walimu vya Kuppet na Knut wanasema ongezeko la maambukizi linaweka walimu na wanafunzi kwenye hatari.

Katika Kaunti za Laikipia, Nyandarua na Baringo, maafisa hao walisema shule zinafaa kufungwa ili kuzuia maambukizi zaidi.

Wiki jana, Waziri wa Elimu Prof George Magoha alisema serikali haina mipango ya kufunga shule licha ya maambukizi kuripotiwa katika baadhi ya shule nchini.

Katibu wa Kuppet tawi la Laikipia, Bw Robert Miano na mwenzake wa Chama cha KNUT wa Nyandarua Kaskazini Maina Kairu walisema kuongezeka kwa maambikizi hayo na vifo mwezi wa Oktoba kunaweka maisha ya wanafunzi na walimu hatarini.

“Kwa sasa tuna walimu 33 kote nchini ambao wameambukizwa virusi vya corona na baadhi ya wanafunzi pia wameathirika. Ni dhahiri idadi ya maambukizi itaendelea kupanda mnamo Novemba ndiyo maana shule zinafaa zifungwe,” akasema Bw Miano.

Waziri wa Afy, Bw Mutahi Kagwe wiki iliyopita, alinukuliwa akisema kwamba taifa linakabiliwa na mkumbo wa pili wa maambukizi hasa baada ya serikali kulegeza baadhi ya masharti yaliyowekwa mwanzoni kuzuia kuenea kwa corona.

Mwenyekiti wa Kuppet tawi la Baringo, Bw David Rotich, pia alisema wanafunzi wa gredi ya nne, darasa la nane na kidato cha nne wanafaa waruhusiwe kurejea nyumbani kuwaepusha na hatari ya kuambukizwa.

“Walimu wana wasiwasi na hawawezi kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Maisha yao na ya wanafunzi wao yana thamani sana. Inasikitisha kwamba vifo na maambukizi yanaendelea kuripotiwa shuleni ilhali serikali imekuwa ikishikilia kwamba haitafunga shule na kuwaruhusu wanafunzi waliorejea mwezi jana warudi nyumbani,” akasema Bw Rotich.

Kauli yake inajiri wiki moja tu baada ya mwalimu shule ya sekondari ya Olmarai, kufariki katika hospitali ya Nakuru baada ya kupatikana na virusi vya corona. Katika kaunti ya Mombasa, mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Tononoka alifariki baada ya kuugua corona.

Visa vya wanafunzi kuambukizwa vimeripotiwa katika shule ya upili ya Maranda, kaunti ya Siaya na shule kadhaa kaunti za Kakamega na Nandi.

Visa 80 vya maambukizi ya corona vimeripotiwa katika Kaunti ya Baringo tangu visa vitano vya mwanzo viripotiwe mjini Marigat mnamo Julai 27.

Mbali na shule, makali ya corona yanaendelea kuripotiwa katika ofisi za umma. Jana, diwani wa wadi ya Kiamokama, Kaunti ya Kisii, Bw Kennedy Mainya alifariki alipokuwa akihamishwa hadi hospitali moja jijini Nairobi.

Bw Mainya alikuwa amelazwa katika hospitali ya Oasis mjini Kisii mnamo Alhamisi ambako aliwekwa kwenye mashini ya kumsaidia kupumua.

Naye Spika wa Bunge la Kaunti ya Machakos Florence Muoti Mwangangi amelazimika kujitenga baada ya kupatikana na virusi vya corona.

Bi Mwangangi ambaye ni mamake Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Mercy Mwangangi alisema kuwa alipatikana na virusi hivyo siku nne zilizopita.

Katika Kaunti ya Nairobi, NMS inatarajiwa kufungua hospitali ya muda yenye vitanda 150 katika hospitali ya Mbagathi ili kukidhi idadi kubwa ya maambukizi ya corona inayoendelea kuripotiwa.