Habari Mseto

Walimu wataka umri wa kuhalalisha ngono uwe miaka 20

June 9th, 2019 1 min read

Na MISHI GONGO

MWENYEKITI wa Chama cha Kitaifa cha Walimu Wakuu wa Shule za Upili, Bw Kakhi Indimuli amependekeza umri wa kuruhusu watu kufanya tendo la ndoa uongezwe hadi miaka 20.

Kulingana naye, ni katika umri huo ambapo hakuna uwezekano wao kukatisha masomo hata msichana akishika mimba.

Aidha amesema chama cha wa walimu hakitasaidia mwalimu yeyote atakayepatikana na tuhuma za kushiriki ngono na mwanafunzi.

Wakati huo huo amesema ni wazimu kuwa na mijadala ya kupunguza umri wa ngono kwani inaashiria kudidimia kwa maadili na kukosa mwelekeo.

Akizumgumza kwenye kongamano la walimu wakuu la 44, katika chuo cha serikali cha ushuru na usimamizi mjini Mombasa Jumapili, mwenyekiti huyo alisema kupunguza umri itakuwa ni kuongeza uozo na kuharibu maisha ya wanafunzi wa kike.

“Hatufai kuwa na mijadala kama hii katika nchi yetu,vipi tuseme msichana wa miaka 16 ni mtu mzima na anaweza kushiriki ngono ilihali akiwa na umri huo bado uko chini ya wazazi na hapaswi kutoa uamuzi wowote bila ruhusa ya wazazi,” alisema.

Aidha mwenyekiti huyo amesema kati ya mada zitakazo jadiliwa katika kongamano hilo ambalo litaanza leo na kuisha ijumaa, ni jinsi ya kudhibiti visa vya wanafunzi kujitoa uhai, mfumo mpya wa elimu na mengineyo.