NA CHARLES WANYORO
KUNDI moja la kutetea haki za walimu wanawake limeitaka wizara ya elimu kuanzishaa vituo vya kunyonyeshea watoto shuleni ili kuhakikisha walimu wapo karibu na watoto wao wachanga katika hatua zao za mwanzo za malezi.
Muungano wa Walimu Wanawake Nchini (Kewota) unasema kwamba sheria ilipitishwa 2016 ikiitaka serikali kujenga vituo hivyo katika taasisi zote za umma lakini shule za umma bado hazijazingatia sheria hiyo.
Mkurugenzi wa Kewota, Benta Opande, alisema walimu wa kike hasa walio na watoto wachanga hulazimika kwenda nyumbani mara kwa mara shule zinapofunguliwa ili kunyonyesha na hivyo kupoteza wakati na pesa.
“Tunataka kusaidia walimu wanawake walio na watoto wachanga na wanaohisi haja ya kwenda nyumbani kuwanyonyesha,” alisisitiza Bi Opande.