Walimu watakaosahihisha KCPE watakuwa katika mazingira salama – Magoha

Walimu watakaosahihisha KCPE watakuwa katika mazingira salama – Magoha

Na SAMMY WAWERU

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha amehakikishia taifa kuwa walimu watakaosahihisha mtihani wa kitaifa kidato cha nane, KCPE watakuwa salama.

Prof Magoha alisema Jumatano, baada ya mtihani huo kukamilika kote nchini, kwamba mazingira watakayokuwamo wasahihishaji yatakuwa salama.

Waziri huyo aliondoa shaka iliyoibuliwa na walimu na wadau husika katika sekta ya elimu, kuhusu usalama wao wakati wa kusahihisha mitihani kipindi hiki taifa na ulimwengu unahangaishwa na virusi hatari vya corona.

“Mitihani lazima isahihishwe. Ninahimiza Wakenya wapuuzilie mbali fitina zinazosambazwa kuhusu usalama wa walimu watakaoendesha mchakato huo. Usalama wao umeangaziwa,” akasema Prof Magoha.

Waziri huyo alisema hayo baada ya kuzuru Shule ya Msingi ya Manyatta, Kaunti ya Kisumu, kutathmini somo la mwisho lilivyofanywa.

“Lolote likitokea wakati wa usahihishaji wa mitihani, tutaliangazia na kulitatua,” Prof Magoha akaelezea.

Kalenda ya masomo nchini mwaka uliopita, 2020 ilisambaratishwa na mkurupuko wa virusi vya corona, ambapo shule na taasisi zote za elimu zilifungwa kwa muda wa mwaka mmoja.

Hatua hiyo ilichukuliwa na serikali ili kuzuia maenezi ya corona miongoni mwa wanafunzi shuleni.

Aidha, zilifunguliwa rasmi Januari 2021.

Watahiniwa wa KCPE na mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE hata hivyo walirejea shuleni Oktoba 2020 ili kujiandaa.

KCPE 2020 imefanywa juma hili, kati ya Jumatatu, Machi 22 – 24.

Watahiniwa wa KCSE 2020 wanatarajiwa kuanza kufanya mtihani Ijumaa, Machi 26, 2021, na watachukua kipindi cha muda wa mwezi mmoja hivi.

You can share this post!

KTDA yabishana na Rais kuhusu chaguzi za wakuu viwandani

Kampuni yashtakiwa kwa kuharibu mti wa Raila