Habari Mseto

Walimu watishia kususia mafunzo kuhusu mtaala

April 21st, 2019 1 min read

Na George Odiwuor

WALIMU katika Kaunti za Kisumu na Homa Bay wameunga mkono hatua ya Katibu Mkuu wa Muungano wa walimu (KNUT) Wilson Sossion kupinga utoaji mafunzo kuhusu mtaala mpya wa elimu (CBC).

Walimu katika kaunti hizo wamepinga mafunzo hayo yanayofaa kuendeshwa na Wizara ya Elimu, wakati serikali inapanga kuanzisha rasmi utekelezaji wa mtaala huo wa elimu.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza Aprili 23, yakilenga walimu 100,000, lakini viongozi wa KNUT Kaunti ya Homa Bay na KUPPET Kaunti ya Kisumu wamepinga mafunzo hayo, wakisema shule nyingi hazina miundomsingi ya kufanikisha mtaala huo.

Katibu Mkuu wa KNUT Homa Bay Cornel Ojuok alisema shule nyingi eneo hilo hazina walimu wa kutosha kuwezesha utekelezaji wa mradi huu. Aliitaka serikali kuajiri walimu kabla ya kuzindua mradi huu,” akasema Bw Ojuok.

Alilaumu serikali kwa kukosa kuajiri walimu kuwezesha ufanikishaji wa mtaala huo.

Aidha, Bw Ojuok alilaumu wizara ya elimu “kwa kuingiza sheria mpya bila kushauriana na walimu” akiwataka wanachama wa muungano huo kutohudhuria mafunzo yanayotarajiwa kuanza wiki hii.

“Wizara inatarajia walimu wahudhurie mafunzo vipi bila kuwapa pesa za kufadhili hilo. Tunawashauri walimu kutohudhuria mafunzo hayo,” akasema Bw Ojuok.

Katibu Mkuu wa KUPPET Kaunti ya Kisumu Zablon Awange naye alihoji kuwa mtaala unaoanzishwa na serikali utaathiri likizo ya walimu na sikukuu za pasaka.