Habari za Kaunti

Walimu watoa ushauri kwa wasichana wanaonyanyaswa kingono

April 25th, 2024 1 min read

GEORGE ODIWUOR Na CHARLES WASONGA

WALIMU katika kaunti ndogo ya Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay wamejiunga katika mpango wa kutoa uhamasisho kwa wasichana matineja ili kuwasaidia kukabiliana na changamoto za kijamii wanazokumbana nazo.

Walimu hao kutoka kata ya Nyokal, wanashirikiana na shirika la Nyokal Women Network katika kuendesha mpango wa kuwapa wasichana hao ufahamu kuhusu haki zao likiwemo la kufanya maamuzi kuhusu masuala ya kimapenzi.

Wasichana wengi katika kaunti hiyo ndogo ya Ndhiwa na sehemu nyingine za Kaunti ya Homa Bay huhadaiwa na wanaume na kupachikwa mimba za mapema kutokana na ufahamu finyu kuhusu haki hizo.

Wengi wao huishia kuathirika na Ukimwi na maradhi mengine ya zinaa.

Kulingana na Bi Margaret Aswani ambaye ni afisa wa mipango katika shirika hilo la Nyokal Women Network, idadi kubwa ya wasichana matineja ambao haki zao huhujumiwa hufeli kuripoti visa hivyo mapema.

“Nyakati nyingine wengine hupata ujauzito na hufichua madhila yaliyowapata miezi kadha baada ya wao kuathirika. Wengine hufichua madhila yao baada ya kugundua kuwa wameambukizwa magonjwa ya zinaa na wamelemewa,” Bi Aswani akasema.

“Hata baada ya wao kujitokeza na kusema walidhulumiwa, wengine hudinda kuwatambua wahusika ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watu hao,” akaongeza.

Ni kutokana na sababu hii ambapo shirika la Nyokal Women Network liliamua kuwahusisha walimu hao.

Kundi la walimu 64 kutoka shule 32 za msingi waliteuliwa kupiga jeki mpango huo wa kuwasaidia wasichana waliobaleghe.