HabariSiasa

Walimu waunga mkono wabunge SRC ivunjwe

June 9th, 2019 2 min read

Na MWANDISHI WETU

CHAMA cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) kinataka Tume ya Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC) ifutiliwe mbali.

Kulingana na Katibu Mkuu wa KNUT, Wilson Sossion, ambaye pia ni Mbunge Maalum, SRC inaleta utata na hali ya kutoelewana kwenye mashauriano kuhusu mishahara kati ya vyama vya wafanyikazi na waajiri.

“SRC inapasa kufutiliwa mbali ili kuokoa pesa za umma kwani kuwepo kwake kunaleta utata kati ya waajiri na wafanyikazi,” akasema Bw Sossion kwenye ujumbe wake kwa Kongamano la Kitaifa la Walimu Wakuu wa Sekondari (KESSHA) linaloanza Jumatatu jijini Mombasa.

SRC pia inakabiliwa na shinikizo kutoka kwa wabunge ambao wamekasirishwa na hatua yake kupinga malipo yao ya marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mwezi.Kulingana na Bw Sossion, Hazina Kuu ndiyo inayopaswa kuchukua jukumu la kusimamia masuala ya mishahara ya walimu, lakini mikataba ya malipo iendelee kuwa kati ya vyama vya walimu na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC).

Bw Sossion pia amependekeza kuanzishwa kwa jopo kushughulikia masuala ya kinidhamu ya walimu pamoja na masuala mengine kama vile kusajili walimu, kuidhinisha vyuo vya mafunzo ya walimu, kusimamia udumishaji wa ubora wa masomo miongoni mwa mapendekezo mengine.

Naye Mwenyekiti wa KESSHA, Bw Indimuli Kahi anataka Serikali kuongeza mgao wa karo inayolipia wanafunzi katika shule za umma kwenye mpango wa Elimu Bila Malipo (FSE) akisema bei ya bidhaa imeongezeka kwa kiwango kikubwa.

“Mgao tunaopata uliwekwa 2014 lakini hautoshi kutokana na gharama ya juu ya maisha. Tunahimiza Serikali itathmini upya mgao huo ili kuhakikisha unatosheleza mahitaji,” akasema Bw Indimuli kwenye ujumbe wake kwa wanachama.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa shule nyingi zinakabiliwa na matatizo ya uhaba wa miundomsingi hasa madarasa na vyumba vya malazi, hali ambayo imesababisha misongamano mikubwa katika shule hizo.

Alieleza kuwa hali hii imetokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi waliojiunga na Kidato cha Kwanza mwanzoni mwa mwaka huuu. Aliomba Serikali kuchukua hatua za haraka kusaidia ujenzi wa madarasa, vyumba vya malazi na mijengo mingine muhimu kwa mafunzo.

Kuhusu mfumo mpya wa elimu, Bw Indimuli alisema walimu wakuu wanataka Serikali ianze kuandaa shule za upili kwa ajili ya kutekeleza mtaala mpya wakati wanafunzi watakapokuwa wakiingia sekondari.

“Tunahimiza Wizara ya Elimu kuanza kuandaa shule za sekondari kwa ajili ya kutekeleza mtaala mpya kwa kuangazia vifaa na mafunzo ya walimu wanaohudumu kwa sasa na walio vyuoni,” akasema Bw Indimuli.