Habari Mseto

Walimu wote kupimwa kabla ya shule kufunguliwa

July 5th, 2020 1 min read

Na GEORGE MUNENE

WALIMU wote watapimwa virusi vya corona kabla ya shule kufunguliwa kama sehemu ya juhudi za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-16.

Waziri wa Elimu George Magoha jana alisema baada ya hapo watakuwa wakipimwa corona kila baada ya wiki mbili.

Akiongea katika Chuo cha Mafunzo ya Utawala (KSG) mjini Embu, Profesa Magoha pia alisema wakufunzi wa vyuo vya walimu (TTC) pia watapimwa kabla ya vyuo hivyo kufunguliwa Septemba mwaka huu.

Waziri aliamuru kuwa sharti walimu wapimwe wiki mbili kabla ya shule kufunguliwa.

Profesa Magoha alimwamuru Katibu wa Wizara hiyo Belio Kipsang’ kuandaa mipango ya namna shughuli hiyo itaendeshwa

“Lazima tuchukue tahadhari ya kuzuia maambukizi kabla ya shule ya vyuo kufunguliwa,” akasisitiza.

Aidha, alikariri kuwa masomo yatarejelewa tu baada ya serikali kuridhika kuwa mikakati ya kuzuia kuenea kwa virusi hivi imewekwa katika shule na taasisi zote za elimu.

Profesa Magoha aliwaagiza wasimamizi wa shule kuhakikisha kuna maji katika majengo yote na vyoo ni safi.

“Shule zinapasa kuwa na maeneo mengi ya kuosha mikono ili watoto wadumishe usafi wa kiwango cha juu nyakati zote.

Profesa Magoha alisema wanafunzi pia watahitajika kudumisha kanuni ya kutotangana.

Waziri alisema hayo wakati ambapo Rais Uhuru Kenyatta leo anatarajiwa kuhutubia taifa kuhusu hali ya janga hilo nchini.