Habari Mseto

Walinzi wapewe bunduki, asema Atwoli

January 16th, 2019 1 min read

NA MWANDISHI WETU

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Kenya (COTU), Francis Atwoli analitaka Bunge kupitisha sheria itakayowaruhusu walinzi kutumia bunduki wanapolinda majengo na makazi mbalimbali.

Bw Atwoli alisema kuwa kuna uwezekano kuwa shambulio la kigaidi katika hoteli ya Dusit mnamo Jumatatu lingethibitiwa kwa haraka, ikiwa walinzi waliokuwepo wangekuwa na bunduki.

Akiwahutubia wanahabari jijini Nairobi Jumatano, katibu huyo alisema kwamba imefikia wakati Kenya kupitisha sheria hiyo haraka, hasa katika nyakati hizi ambapo visa vya ugaidi vinaendelea kuongezeka.

“Enzi za walinzi kutumia rungu pekee kuendesha shughuli za usalama zimepitwa na wakati. Imefikia wakati tuwaruhusu kutumia bunduki ili kuzuia maafa na uharibifu wa mali wakati mashambulio kama hayo yanapotokea,” akasema Bw Atwoli.

Alitoa mfano wa nchi kama Uganda, Rwanda na Ethiopia, ambapo walinzi ambao hulinda hata mikahawa midogo huwa wanamiliki bunduki.

Alimtaka Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i kusaidia katika uharakishaji wa mchakato huo akisema utachangia pakubwa katika kuimarisha usalama wa Wakenya.

Alisema kuwa kuna uwezekano kwamba Wakenya wengi wangeokolewa, ikiwa walinzi hao wangekuwa na bunduki, kwani wangewakabili magaidi kabla ya kutekeleza mauaji zaidi.

“Utathmini wa kina unaonyesha kwamba Wakenya wanaomiliki bunduki ndio waliofika haraka na kuanza kuwaokoa wale waliokuwa wakishambuliwa,” akasema.