Habari

Walinzi wapewe bunduki, PSRA yapendekeza

June 12th, 2019 2 min read

NA CECIL ODONGO

MAMLAKA ya Kusimamia Shughuli za Walinzi wa Kibinafsi Nchini (PSRA) sasa imependekeza walinzi wanaolinda maeneo spesheli wapewe bunduki ili kutokomeza visa vya utovu wa usalama.

Afisa Mkuu Mtendaji PSRA Fazul Mohamed Jumatano amesema sheria ya sasa inayoharamisha walinzi kupokezwa bunduki inafaa kubadilishwa ili wale wanaolinda maeneo maalum kama benki, maduka ya jumla, hoteli maarufu na watu wanaotambulika wapewe silaha hizo kutekeleza wajibu wao.

“Unatarajia vipi mlinzi aliyejihami kwa rungu kumkabili gaidi wa Al Shabaab ambaye amejihami kwa silaha hatari? Tunataka sheria ibadilishwe ili walinzi wa maeneo spesheli wapewe bunduki wanapokuwa kazini.

“Walinzi wetu hutoa huduma bora katika nchi nyingine duniani na hata hutamba kwenye mashindano ya nje lakini hapa nchini hatuwathamini na kazi zao,” akasema Bw Mohamed.

Mnamo Januari 2019, Bw Mohamed alitangaza kwamba walinzi wa kibinafsi wanaolinda sehemu hizo maalum wangepokezwa bunduki baada ya miezi sita ya mafunzo kabambe ila hilo litatimia tu baada ya sheria inayowazuia kupewa bunduki kubadilishwa bungeni.

Aidha alitaka kampuni za kibinafsi na watu waliowapa ajira walinzi kuhakikisha wanawalipa mishahara mizuri badala ya kuwanyanyasa kutokana na dhana ya tangu zamani ya kuwadunisha walinzi kwa malipo ya mlalahoi.

“Kampuni ambazo zinaweza kuwalipa walinzi vizuri zimekataa kufanya hivyo kimakusudi kwasababu zinaweza kupata huduma hizo kwa malipo ya chini kwingineko.

“Inawezekanaje mlinzi wa benki analipwa Sh4,000 au 5,000? Na analinda jengo zima yenye umuhimu mkubwa. Hali hii ndio huchangia baadhi ya walinzi kushirikiana na wakora ambao huwapa pesa kidogo na kutekeleza mashambulizi.

“Pia kuna kampuni ambazo zinaendelea kuleta walinzi kutoka nje, tunawapa siku 60 kuhakikisha kwamba wanawaajiri walinzi kutoka Kenya. Kabla ya kutoa walinzi kutoka nje lazima watushawishi ili tuwaruhusu kufanya hivyo maana kuna walinzi wataalam nchini,” akaongeza Bw Mohamed katika mkahawa wa Laico Regency wakati wa mkutano wa Muungano wa Wakazi wa Jiji la Nairobi (KARA).

Sekta ya ulinzi wa kibinafsi inatoa ajira kwa karibu Wakenya 500,000 huku taifa likijivunia karibu kampuni 2,500 za kutoa huduma za ulinzi nchini.

Wakati wa mkutano huo, kulikuwa na pendekezo la mtaala unaoongoza mafunzo ya walinzi yaimarishwe pamoja na mazingira yao ya kufanya kazi.