Makala

Walio na upofu wajifunza kazi za mkono kuepuka kuwa ombaomba

February 9th, 2024 3 min read

NA LABAAN SHABAAN

MJASIRIAMALI mbunifu anayesaka tonge kwa kutengeneza bidhaa za karatasi ya khaki, Charles Kimani, ameishia kuwa wakala wa kuhifadhi na kunadhifisha mazingira mbali na kujenga jukwaa la watu wanaoishi na ulemavu kujitafutia riziki na kuepuka kugeuka ombaomba. 

Saa nane adhuhuri katika mtaa wa Witeithie, eneobunge la Juja, Kaunti ya Kiambu, karakana ya Jamii Products, inaendeleza mafunzo ya stadi ya kazi za mkono kwa wanafunzi wenye ulemavu wa macho wenye ndoto kubwa ya kustawi kiuchumi.

Wanafunzi Anne Thuo,46, Philip Wambua,48, na James Karanja,68, ni miongoni mwa makumi wanaojifunza kazi hii ili wajibunie ajira.

Taifa Leo iliwakuta wakitengeneza vifurushi vya kupakia vitu kama vile sukari, mchele, unga na kadhalika.

Watatu hawa wana ulemavu wa macho na hutembea kwa mikongojo maalum kuwezesha mwendo.

Walivutiwa na kituo hiki ambacho kimekuwa kimbilio kwa watu wanaoishi na ulemavu wanaosaka njia ya kuanzisha biashara zao ili wajitegemee.

“Wale wanaoenda barabarani kuomba wanafaa kujifunza kazi hii sababu pesa watakazopata zinaweza kuwa nyingi,” alisema Bi Thuo akiongeza shughuli hii ni muhimu kuondoa upweke na kukaa bure.

Miaka 20 iliyopita, Bw Karanja aliugua glakoma, ugonjwa uliompofusha na kuyumbisha matumaini yake ya kujisimamia.

“Nimeona hakuna haja nikae nyumbani kutegemea kuletewa kwa kuonewa huruma. Nikiwa na kazi ya mikono ambayo inaweza kunisaidia ni afadhali,” aliambia Taifa Leo.

Wanafunzi hawa wanavutiwa na mpango wa mwasisi wa kituo hiki ambaye wengi wamempa lakabu ya Kimani wa Karatasi.

Mwasisi wa Jamii Products  Charles Kimani atengeneza kiti kutokana na uchafu wa khaki. PICHA | LABAAN SHABAAN

Yeye kuwapiga jeki wanaoishi na ulemavu kujianzishia vyanzo vya kupata mkate wa kila siku.

Mwanafunzi binafsi akiingia hapa kujisajili, Jamii Products huwafunza bila malipo.

Walio kwenye vikundi hufunzwa wakilipa Sh300 pekee; kiwango kidogo ikilinganishwa kama wangelipa karo ya kawaida ya kiwango cha Sh15,000.

“Tumetoa mafunzo kwa makumi ya makundi ya wanaoishi na ulemavu. Baada ya mafunzo, wasamaria wema huwasaidia,” akasema Bw Kimani akifunguka kwa Baraza la Kitaifa la Wanaoishi na Ulemavu (NCPWD) hutoa mtaji wa Sh80,000 kwao kuanza biashara.

Bw Kimani anaeleza kuwa mwenye nia ya kuanza biashara hii anaweza kutumia mtaji wa angalau Sh10,000.

Mahitaji muhimu ya kazi hii yanahusisha vifaa kama vile makasi zigizagi, vipande vya mbao, bodi, gundi na malighafi.

Kwa kweli, imesadifu elimu ni bahari yenye upeo ambao huwezi kuufikia.

Wanafunzi wenye umri uliosonga wameona mbele na wana imani tele kuwa ulemavu si udumavu wala kutojiweza.

“Hakuna kitu mikono haiwezi kufanya. Inaweza hata kumuumba binadamu: ni uhai tu haiwezi kumpa. Walemavu na wasio na ulemavu, wote wako sawa,” aliungama Bi Thuo.

Mwanafunzi mwenzake Bw Karanja akadokeza: “Nina mpango wa kujisaidia kutumia kazi hii na pia kusaidia watoto wangu. Niliwaeleza kuhusu kazi hii zamani lakini hawakushughulika.”

Pindi watakapomaliza kisomo chao cha majuma mawili, watafikisha masokoni bahasha, boksi za keki, majalada ya vitabu, vifurushi vya kupakia zawadi na bidhaa nyingine.

Bw Kimani alianza kituo hiki mwaka wa 2018 baada ya serikali kupiga marufuku mifuko ya plastiki kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Anaeleza alikuza karakana hii kwa mtaji wa mikopo ya simu na msaada wa familia akikutana na viunzi alivyofaulu kuviruka.

“Wakati huo nilikuwa ninafanya majaribio nikishindwa katika safari ya kugundua nilichoweza kufanya nikiwa mwanachuo wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia (Jkuat),” alipasua mbarika.

“Nilikuwa ninatafuta biashara ambayo ingenisaidia kumudu maisha ili nisiwe mtu wa kuombaomba watu waniepuke,” aliongeza.

Mjasiriamali huyu ameondokea kuwa wakala wa mchakato endelevu wa kuhifadhi mazingira.

Amekweza jamii katika nafasi ya kuepuka matumizi ya mifuko ya plastiki na badala yake kutumia vifurushi vya khaki visivyo hatari kwa mazingira.

Kadhalika, uchafu unaobakia baada ya kutengeneza bidhaa hizi bado ni muhimu kuunda vitu vingine.

Mabaki ya mchakato wa kuzalisha bidhaa hutumiwa kuunda vigoda vidogo, vesi za maua, vishikio vya taa, mikwaju, kutaja tu baadhi.

“Baada ya serikali kupiga marufuku mifuko ya sandarusi, niliona nafasi ya kibiashara na pia ya kuletea jamii suluhu ya matatizo ya uchafuzi wa mazingira,” Bw Kimani aliambia Taifa Leo.

Takriban kilomita 10 kutoka Witeithie, katika eneo la Nyacaba, mmoja wa wanafunzi wa zamani, Irene Muthoni, hutumia stadi aliyopata baada ya kuanza kwa mtaji wa Sh25,000.

“Hii ni kazi nzuri kwa sababu inanisaidia kulipa bili zangu na sitaabiki kumudu gharama ya maisha,” alisema Bi Muthoni ambaye ni mama wa watoto wawili.

Sawa na Bw Kimani, mjasiriamali huyu pia anaendeleza mafunzo kwa wengine wanaomezea mate biashara hii ya kazi ya mikono isiyohitaji vyeti vya elimu.

Huwa furaha kwa mwasisi wa Jamii Products wakati wanafunzi waliopata utaalamu huu wanaanza biashara zao.

“Njia yangu ya kujua matokeo ya mafunzo ninayotoa  ni wakati wanakuja kwenye bohari langu kununua malighafi ya kutengeneza bidhaa,” Bw Kimani aliungama.

Juhudi za Bw Kimani kujibunia mbinu ya kujitegea uchumi ili kujitegemea, zimezaa baraka maradufu.

Zimetengeneza jukwaa la wengine kujichumia senti na pia kuwa mhimili muhimu wa kuhifadhi mazingira.