Habari Mseto

Walioasi Al Shabaab sasa wajiunga na magenge Pwani

April 29th, 2019 2 min read

Na MOHAMED AHMED

VIJANA waliojiondoa katika kundi la kigaidi la Al Shabaab na kurudi humu nchini sasa wanajiunga na magenge ya ujambazi yanayovamia maduka ya kibiashara eneo la Pwani.

Vijana hao, kulingana na habari za ujasusi, ndio wamekuwa wakihusika katika visa vingi vya ujambazi katika kaunti ya Mombasa na Kwale ambapo wameweka maficho yao.

Miongoni mwa sababu kuu za kujiunga na magenge hayo ni kuwa katika ukanda wa Pwani, hakuna hata kituo kimoja cha kurekebisha tabia za vijana hao licha ya serikali kuwasisitizia wajisalimishe.

Ripoti za vijana kujiunga na magenge ya majambazi zinakuja baada ya majambazi watatu kuuawa Jumapili wiki jana na mmoja wao kutambulika kuwa alikuwa ni miongoni mwa vijana wanaohusishwa na kundi la kigaidi.

Kijana huyo aliyetambuliwa kwa jina la Mwidani alikuwa miongoni mwa watatu waliouawa eneo la Mariakani baada ya kuwaibia wafanyabiashara wawili Sh660,000. Mwingine aliyeuawa ni Simon Kinyua ila wa tatu hajatambulika jina lake.

Walikuwa kwenye genge la watu wanne na mmoja wao, Juma Karisa ambaye aliponea kifo, kukamatwa na kufikishwa katika mahakama ya Mariakani ambapo maafisa wa polisi waliruhusiwa kumzuia kwa muda wa siku 14.

Maafisa wa polisi kutoka kitengo cha kupambana na ugaidi (ATPU) walienda na Karisa kwa ajili ya mahojiano ya kina.

Bunduki mbili aina ya AK47 pamoja na risasi 59 zilipatikana kutoka kwa majambazi hao.

Kabla ya tukio hilo, genge jingine linaloaminika kuhusiana na hilo liliwaua kwa kuwapiga risasi maafisa wawili wa polisi eneo la Diani, Kaunti ya Kwale wiki mbili zilizopita.

“Mauaji ya maafisa hao yalikuwa yamefichwa baada ya kujulikana kuwa waliohusika ni vijana hao waliokuwa kwenye makundi ya ugaidi na kurudi,” akasema mdokezi wetu.

Mapema mwaka huu, mwenyekiti wa kamati ya usalama wa Pwani Jogn Elungata alisema kuwa vijana hao wamekuwa wakijiunga na magenge ya uhalifu kuendeleza itakadi zao. Kamishana wa Mombasa, Bw Evans Achoki, aidha, aliungama kuwa hakuna hata kituo kimoja cha kurekebisha tabia za vijana hao ambao wengi wamerudi kutoka nchini Somalia.

Badala yake, wiki jana serikali ya Kenya ilipata ufadhili kutoka kwa serikali ya Uingereza unaolenga kuwajengea kituo cha kitengo cha ATPU kwa gharama ya Sh60 milioni.

Mkurugenzi wa kitengo cha upelelezi (DCI) George Kinoti alisema kituo hicho kitasaidia kuzivunja njia zinazotumika kuwaingiza vijana katika makundi haramu ya ugaidi enoe la Pwani.

“Tumeleta juhudi zetu karibu huku Pwani ambapo hatari kubwa imeonekana kuwepo. Kituo hiki kitatusaidia pakubwa kupambana na masuala ya ugaidi katika hali ya kitaifa kwa sababu ya vifaa ambavyo tutakuwa navyo,” akasema Bw Kinoti aliyekuwa ameandamana na Balozi wa Uingereza nchini Kenya Nic Hailey.

Bw Hailey alisema kuwa ugaidi umesalia kuwa tishio kwa mataifa yote ulimwenguni na ni kwa kuhami vyombo vya usalama tu ndipo mapambano na janga hilo yakapofaulu.