WALIOBOBEA: Kosgey; Waziri msiri na mwaminifu kwa Kibaki

WALIOBOBEA: Kosgey; Waziri msiri na mwaminifu kwa Kibaki

KWA HISANI YA KYB

MOJAWAPO ya sifa za Henry Kiprono Kosgey ni uaminifu na aliudumisha vilivyo.

Na hii ni sifa ambayo Mwai Kibaki anapenda sana na inaweza kuelezea kwa nini Rais wa tatu wa Kenya alikuwa akimpenda Kosgey aliyesomea Chuo Kiku cha Nairobi na ambaye alijiuzulu kutoka kampuni ya Kenya Breweries Limited kujiunga na siasa mwaka wa 1979.

Kosgey alikuwa mwandani wa karibu wa Rais Daniel Moi ilivyodhihirishwa na nyadhifa sita za uwaziri (ikiwemo Uchukuzi na Mawasiliano, Utamaduni na Huduma za Jamii, Elimu na Ustawi wa Vyama vya Ushirika) alizohudumu katika serikali ya chama cha Kenya African National Union (KANU) kati ya 1979 na 2002.

“Nilikuwa mwanafunzi mzuri wa Moi na mwaminifu kwa serikali. Bila yeye, singejiunga na siasa,” Kosgey alisema Machi 2020 kwenye mahojiano na gazeti la Daily Nation.

Kulingana na ufichuzi wa Wikileaks Cables, “ingawa (Kosgey) ni mwanachama wa jamii ndogo ya Nandi na sio ( ya aliyekuwa rais Daniel arap) Moi ya Tugen, kwa miaka mingi alikuwa mwandani wa karibu na aliyeaminiwa na rais huyo wa zamani.”

Hii inaeleza kwanini Kosgey alichagua kubaki na kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga ingawa baada ya 2008, mazingira ya kisiasa katika jamii yake ya Kalenjin yalibadilika kuelekea William Ruto, ambaye alikuwa ametofautiana na kiongozi huyo wa ODM.

Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba uaminifu wake haujawahi kuondoa hisia zake za kujinusuru. Ni mwaminifu ndio. Lakini pia mwanasiasa mwerevu wa kusoma ishara za wakati, ilivyokuwa wakati huo.

Kanu iliposhindwa kwenye uchaguzi mkuu wa Desemba 2002, Kosgey alihama chama chake cha kisiasa alichohudumia kwa miaka mingi na kujiunga na ODM. Kosgey, sawa na alivyo Kibaki, ni mtulivu na muungwana lakini wote wawili ni wagumu kama chumba kwa ndani.

Kama Kibaki, Kosgey alikuwa mbunge akiwa na umri wa miaka 32. Wote wawili waliacha waliacha kazi zao- Kibaki aliacha kazi katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda naye Kosgey aliacha kazi Kenya Breweries Limited — kujiunga na ulimwengu wa siasa. Na wote walidumu kwa muda mrefu katika siasa na ni miongoni mwa wabunge waliohudumu kwa miaka mingi nchini Kenya( Kibaki alikuwa mbunge kwa miaka 50; na Kosgey kwa miaka 29).

Kosgey alikuwa miongoni mwa wanasiasa wachache waliojaliwa kuhudumu katika serikali za Moi na Kibaki wakiwa Mawaziri. Wengine walikuwa Odinga, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, Simeon Nyachae, William ole Ntimama na Dalmas Otieno. Alikuwa miongoni mwa viongozi wa upinzani waliosaidia kutuliza nchi ghasia za baada ya uchaguzi mkuu za 2007–2008 zilipozuka.

Na Kibaki alikuwa akimpenda Henry Kosgey na alitaka awe katika Baraza lake la Mawaziri hivi kwamba mnamo Septemba 2006 alituma wajumbe kwa Kosgey (wakati huo alikuwa makamu mwenyekiti wa Kanu) kumshawishi ajiunge na serikali ya National Rainbow Coalition (NARC). Kosgey alikataa.

“Nikiwa awali nilihudumu katika wizara tofauti kwa miaka 15, niliwauliza (wajumbe) kunieleza wizara ambayo Kibaki alikuwa amenitengea. Hawakuwa na jibu,” aliambia gazeti la Sunday Nation kwenye mahojiano Septemba 2006.

Kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka wa 2008, Kosgey aliyekuwa mbunge wa Tinderet aliteuliwa waziri wa Viwanda. Waziri wake msaidizi akiwa Ndiritu Muriithi.

Alikuwa mmoja wa Wakenya sita walioshtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu ICC kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu za 2007-2008 kabla ya mashtaka kuondolewa na akawa huru.

Amegombea kiti cha useneta kaunti ya Nandi mara mbili akishindwa.

You can share this post!

SOKOMOKO: Hii tufani ya Mudavadi ipo kweli ama ni majitapo...

AFCON: Salah abeba Misri dhidi ya Guinea-Bissau katika...

T L