Afya na JamiiMakala

Waliochafua jiji kwa haja ndogo waamrishwa kusafisha mochari


WATU 30 waliokamatwa mnamo Jumatatu, Agosti 19, 2024 wakichafua jiji la Nairobi kwa kuenda haja ndogo barabarani wamepewa adhabu ya kutoa huduma kwa jamii, ikiwemo kusafisha chumba cha kuhifadhia maiti.

Mahakama moja ya Nairobi, mnamo Jumanne, Agosti 20, 2024, iliamuru kuwa baadhi ya wachafuzi hao wakisafishe chumba cha kuhifadhi maiti cha Nairobi Funeral Home (awali kikijulikana kama City Mortuary) na kufagia baadhi ya vyunga vya jiji hilo kuu.

Wengine waliamrishwa kunadhifisha bustani ya Uhuru Park.

Walianza kufanya kazi hiyo Jumatano, Agosti 21, 2024.

Waliopewa adhabu ya kusafisha mochari, walipewa glavu, ndoo za maji na vifaa vingine vya kusugua na wakaelekezwa kuhakikisha mochari hiyo inang’arishwa vilivyo.

30 hao walikamatwa kufuatia msako uliofanikishwa na maafisa kutoka Idara ya Mazingira ya Kaunti ya Nairobi.

Maafisa wa kutekeleza amri za kaunti na wale wa Idara za Afya na Mazingira, walihakikisha usafi katika mochari hiyo unatekelezwa kwa uangalizi mkubwa.

Afisa Mkuu wa Idara ya Mazingira wa Kaunti ya Nairobi Geoffrey Mosiria aliongoza zoezi hilo.

Alimshukuru hakimu aliyetoa uamuzi huo, na kuongeza kuwa uamuzi wake utatumika kama funzo kwa wale wenye mazoea ya kuvunja sheria.

“Ni vibaya kwa watu kuenda haja ndogo na kutupa taka popote katikati mwa jiji,” Bw Mosiria alisema.

Aliwasihi wakazi wa Nairobi kujifahamisha na sheria na kanuni zinazoongoza kaunti hiyo.

Kulingana na mojawapo ya kanunu za jiji la Nairobi za mwaka 2021, kuenda haja ndogo au kubwa hadharani kunaweza kumletea mtu faini ya Sh10, 000, kufungwa jela miezi sita au yote mawili.

Kanuni zingine zinahusisha kusafisha pua kwa kutoa kamasi bila kutumia kitambaa spesheli (handkerchief) au karatasi shashi (toilet paper), ambapo mhusika anahatarisha kupigwa faini kati ya Sh10, 000 hadi Sh500, 000 au kifungo cha kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja.

Hii pia inahusisha kutema mate ovyoovyo barabarani, kulala jikoni au katika maghala ya chakula, miongoni mwa tabia zingine za kuchukiza.

Imetafsiriwa na Wycliffe Nyaberi