HabariSiasa

Walioegemea kwa Ruto sasa waapa kuletea ODM ushindi

August 18th, 2019 2 min read

Na SAMUEL BAYA

WABUNGE wawili ambao walikuwa wakimshabikia Naibu wa Rais William Ruto wameamua kumuunga mkono mwaniaji udiwani wa Chama cha ODM katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Ganda, eneobunge la Malindi, Kaunti ya Kilifi.

Mwaniaji wa kiti hicho kwa tiketi ya ODM, Bw Reuben Katana anatarajiwa kumenyana na aliyekuwa diwani wa wadi hiyo, Bw Abdul Omar ambaye ni mwaniaji wa kujitegemea.

Bw Omar ni mshirika wa karibu wa mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa na ushindi wake wa mwaka wa 2017 ulifutiliwa mbali na mahakama baada ya kesi kuwasilishwa na Bw Katana ambaye aliwania wakati huo na chama cha Kadu Asili.

Wabunge hao, Bw Owen Baya (Kilifi Kaskazini) na mwakilishi wa kike kaunti, Bi Gertrude Mbeyu jana waliambia Taifa Leo kwamba watahakikisha kuwa Bw Katana ameshinda kiti hicho.

Tangazo la Bw Baya na Bi Mbeyu linazidi kuonyesha jinsi Bi Jumwa anaendelea kupoteza marafiki kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Baya alisema kuwa ataunga mkono mwaniaji wa ODM akiwa mwanachama wa chama hicho.

“Mimi ni mwanachama wa ODM na niko huru kumuunga mkono mwanachama mwenzetu kuwania kiti hicho. Sijaenda kinyume na matakwa ya chama wala uongozi wake. Ndio maana tuko ndani ya chama miaka yote hiyo,” akasema Bw Baya.

Naye Bi Mbeyu alisema kuwa atabakia kuwa mwanachama wa ODM na ataunga mkono mwaniaji wa chama hicho ashinde kiti hicho.

“Hakuna urafiki au uadui katika siasa. Mimi ni mwanachama wa ODM na nitaendelea kuunga mkono ODM. Huyo mwaniaji wetu lazima ashinde na hata tukiongea saa hii nimetoka Kakamega kushiriki katika kundi letu la Embrace,” akasema Bi Mbeyu.

Hatua hiyo ya Bi Mbeyu imeonekana kutofautianana msimamo wake ambapo amekuwa akiponda uongozi wa ODM huku akishabikia naibu wa Rais na Bi Jumwa.

“Kama rafiki yangu anaweza kuniambia kwamba mimi sina kura za kumwezesha Bw Ruto kuwa Rais, basi wacha aendelee mbele. Ila ninataka kumwambia rafiki huyu kwamba huenda atashangaa na matokeo ya siku za usoni,” akasema Bi Mbeyu.

Naye naibu mwenyekiti wa chama cha ODM katika kaunti ya Kilifi, Bw Teddy Mwambire aliahidi kwamba ODM itashinda kiti hicho.

“Bw Katana sasa amepatiwa cheti cha kuwania kiti hicho cha Ganda. Sasa ni jukumu letu kama wanachama wa ODM pia kuendelea kumsaidia ili kufanikisha azimio letu la kuhakikisha kwamba kiti hicho kimerudi katika himaya ya ODM,” akasema Bw Mwambire.

Aliwataka wanachama wote wa ODM ikiwemo viongozi na wabunge kufika kwa wingi katika eneo hilo na kumpigia debe Bw Katana kuwa diwani wa eneo hilo.

“Nimepata tetesi kwamba kuna baadhi ya wanachama wetu wamekuwa wakisema kwamba huenda wakafanyia kampeini watu ambao hawajulikani katika chama cha ODM. Ninataka kutoa onyo la mapema kwamba tunawafuatilia vyema na wasifikirie kwamba tumelala,” akasema Bw Mwambire.

Uchaguzi huo pia unatarajiwa kumweka Bi Jumwa kwa mizani ambaye anajitahidi kuonyesha umahiri wake baada ya kutangaza kumuunga mkono Bw Ruto.