Walioenda kulipa mahari walimwa faini

Walioenda kulipa mahari walimwa faini

Na JOHN MUSYOKI

SHANZU, Mombasa

VIJANA waliofika katika boma moja sehemu hii kulipa mahari walitozwa faini na wazee wa familia ya kidosho kwa kutoandamana na wazee wa familia yao.

Inasemekana jamaa aliyeoa demu alipuuza wazee wa familia yake na kuwachagua baadhi ya marafiki wake kumwakilisha kwa wakwe zake.

Wakati wa kuandaa kikao cha faragha ulipowadia, wazee wa familia ya demu walishangaza jamaa alipowaleta vijana barobaro kuzungumzia suala nzima la mahari ya binti yao.

Wazee walianza kulalamika wakidai walikuwa wamedhalilishwa na jamaa huyo. “Hawa ndio wazee wako? Unatufanyia mzaha kwa nini? Mbona unatuletea watu wasio wa rika letu kuzungumzia suala la mahari. Marafiki hawa wako wanajua nini kuhusu ndoa na kulipa mahari. Kama unataka msichana wetu rudi ukatuletee wazee wa rika letu,” mwakilishi wa familia ya demu alisema.

Inasemekana jamaa na marafiki wake walizusha lakini waliambulia patupu. “Mnatudharau kwa nini? Haja yenu ni mahari ama ni wazee? Vijana kama sisi tuna uwezo wa kufanya kikao cha faragha kama wazee,” jamaa mmoja aliwaambia wazee.

Inasemekana licha ya vijana hao kujitetea wazee walisisitiza ilikuwa ni mwiko kwa barobaro kuhusishwa na masuala ya kujadili na kulipa mahari. “Mnatupotezea muda. Kulingana na kanuni zetu hatuwezi kuandaa kikao na vijana kama nyinyi. Mnataka laana?” mzee mmoja aliongeza.

Ilibidi jamaa na marafiki wake kufanya walivyoambiwa.

Hata hivyo, hawakuruhusiwa kuondoka boma la wakwe hivi hivi.

“Waliachiliwa kuondoka baada ya kutozwa faini ya Sh30,000 kwa kuwapotea wazee muda,” alisema mdokezi.

You can share this post!

NGILA: Vijana msilaze bongo, mamilioni yawasubiri!

BI TAIFA FEBRUARI 24, 2021