Waliofuja pesa NSSF wapatikana na hatia ya ulaghai wa Sh1.4 bilioni

Waliofuja pesa NSSF wapatikana na hatia ya ulaghai wa Sh1.4 bilioni

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA meneja wa uwekezaji katika Hazina ya Kitaifa ya Mafao ya Uzeeni (NSSF) na wafanyakazi watatu wa kampuni ya kununua na kuuza hisa iliyofilisika, Ijumaa walipatikana na hatia ya ulaghai wa Sh1.4 bilioni.

Kiongozi wa mashtaka aliomba mahakama ya kuamua kesi za ufisadi iwatoze faini ya Sh4.2 bilioni kila mmoja pamoja na kuwasukuma jela kwa kifungo kisichopungua miaka 10.

Hakimu mkuu Bw Lawrence Mugambi aliwapata na hatia Francis Zuriels Moturi (aliyekuwa meneja wa uwekezaki NSSF), David Ndirangu (NSSF) na maafisa wa kampuni ya Discount Securities Ltd (DSL) Wilfred Mungoro (mkurugenzi wa masuala ya fedha) na Isaac Nyakundi (aliyekuwa meneja wa uwekezaji DSL ya kula njama ya kuiba hela ya NSSF wakidai waliwekeza katika hisa.

“Ninaomba mahakama hii iwatoze faini ya Sh4.2 bilioni kila mmoja kwa kula njama ya kuilaghai NSSF Sh1.4 bilioni wakidai wataziwekeza katika biashara ya hisa,” kiongozi wa mashtaka alisihi hakimu mkuu Bw Mugambi.

Bi Hellen Mutela alimweleza Bw Mugambi kuwa chini ya sheria za hujuma za kiuchumi mshtakiwa hutozwa faini mara tatu ya pesa alizoiba.

Lakini mawakili wanaowatetea washtakiwa hao waliomba wapewe muda wa kujitetea.

Bw Mugambi alikubaliana na wakili wa washtakiwa kwamba anahitaji muda wa kuandaa malilio kabla ya adhabu kupitishwa.

“Ili kuwapa muda washtakiwa waandae malilio yao kabla ya hukumu kupitishwa ninaamuru washtakiwa wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Capitol hadi Jumatatu (Januari 31, 2022),” Bw Mugambi aliamuru.

Akisoma uamuzi huo, Bw Mugambi alisema upande wa mashtaka umethibitisha makosa dhidi ya washtakiwa kwa kuwasilisha ushahidi jinsi walivyofyonza NSSF kati ya 2004 na 2007 zaidi ya Sh1.6 bilioni wakidai watawekeza kwa kununua hisa katika kampuni kuu saba nchini.

Moturi aliyestafu kutoka NSSF baada ya kuhitimu miaka 55 mnamo 2005 alipatikana na hatia katika mashtaka matatu.

Wakurugenzi wa DSL Ndirangu, Mungoro na Nyakundi walipatikana na hatia ya kula njama za kulaghai, undanganyifu, ufisadi na wizi.

Lakini mahakama iliwaachilia aliyekuwa meneja mkuu masuala ya fedha na uwekezaji James Akoya na aliyekuwa mkaguzi wa hesabu NSSF Bi Mary Ndirangu na kampuni ya Orchard Estates Ltd. Bw Mugambi alisema washtakiwa hao wanne walikula njama za kuwekeza kupitia kampuni ya DSL iliyofilisika ikiwa na mabilioni ya pesa za umma.

Mashtaka mengine waliyopatikana na hatia ni kulipa pesa za wazee kwa njia ya ufisadi, kutofuata sheria za uwekezaji, kujinufaisha na mali ya umma kwa njia ya ufisadi, wizi na kutozingatia sheria katika usimamizi wa mali ya umma.

Wanne hao walikana walitekeleza uhalifu huo kati ya Agosti 2004 na Julai 20 2007 kwa kudai walinunua idadi kubwa ya hisa kwa niaba ya NSSF.

Mahakama ilifahamishwa NSSF iligeuzwa kuwa hazina ya malipo ya uzeeni 2003 kisha bodi ya wasimamizi wakaamua wawekeze pesa hizo za malipo ya uzeeni katika miradi ya kuiletea NSSF mapato.

Mameneja wa NSSF walipendekeza wawekeze zaidi ya Sh1.6bilioni. Lakini hatimaye wakuu wa NSSF waligudua kupitia uchunguzi wa shirika la uwekezaji (CDSC) pesa hizo (Sh1.6 bilioni) hazikuwekezwa ila zilipotea.

You can share this post!

Raia wateseka siasa zikivuma

STAA WA SPOTI: Spidi yake kali ilimtoa katika voliboli na...

T L