Waliofungwa jela maisha kwa kuficha gaidi wa al-Qaeda waachiliwa huru

Waliofungwa jela maisha kwa kuficha gaidi wa al-Qaeda waachiliwa huru

Na PHILIP MUYANGA

MWANAMUME na mwanawe ambao walihukumiwa kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kumpa makao gaidi wa kundi la al-Qaeda, wameachiliwa huru.

Bw Mahfudh Ashur Hemed na mwanawe, Ibrahim Mahfudh waliachiliwa huru Alhamisi katika Mahakama Kuu ya Mombasa iliyokubali rufaa yao na kuzuia hukumu waliyokuwa wamepewa mwaka wa 2019.

Wawili hao walikuwa wamepatikana na hatia ya kumpa makao Fazul Abdullah ambaye alihusishwa na shambulio la kigaidi lililotokea katika ubalozi wa Amerika jijini Nairobi mwaka wa 1998.

Fazul ambaye aliaminika kuwa mkuu wa al-Qaeda Afrika Mashariki aliuliwa nchini Somalia mwaka wa 2011.

Jaji Anne Ong’injo aliamua kuwa ushahidi uliokuwa umewasilishwa na upande wa mashtaka ulikuwa na mianya tele ambayo haingetegemewa kuwahukumu wawili hao.

Alisema upande wa mashtaka haukuthibitisha kwa kiwango cha kuridhisha kuwa Fazul alikuwa amefichwa katika nyumba ya wawili hao.

Mahakama ilisema mashahidi wawili wa upande wa mashtaka walitoa ushahidi kuhusu jinsi walivyopokea habari kuwa washukiwa sugu wa kigaidi waliokuwa wakitafutwa walikuwa wanaishi Malindi na mdokezi wao alimtambua mmoja wa washukiwa hao.

Hata hivyo, mahakama imesema mdokezi huyo ndiye angetoa ushahidi wake mahakamani au angewasilisha hati ya kiapo kuhusu aliyodai kuyashuhudia.

Jaji Ong’injo pia aliuliza kwa nini kifaa cha kunyoa nywele ambacho upande wa mashtaka ulisema kilitumiwa kupata chembe za DNA za Fazul, kilichosemekana kupatikana katika nyumba ya wawili hao, hakikuchukuliwa na polisi waliovamia nyumba hiyo.

Katika ombi lao la rufaa, walisema hakimu alifanya makosa kisheria kuendeleza kesi hadi kuwahukumu kwa kutegemea mashtaka yaliyokuwa na kasoro.

Hukumu ya kuwafunga ilikuwa imetolewa na aliyekuwa hakimu mkuu wa mahakama ya Mombasa, Bw Maxwell Gicheru ambaye kwa sasa ni jaji.

Fazul alikuwa amehusishwa pia na shambulio la kigaidi lililotokea Kikambala, Kaunti ya Kilifi katika mwaka wa 2002.

Alisemekana kuwa nchini katika siku ambazo hazijabainika, kati ya Desemba 2007 na Agosti 2, 2008 katika mtaa wa Silversand, Malindi.

You can share this post!

WASONGA: Knut, Kuppet zisitishe migomo wakati huu

MATHEKA: Kuahirisha uchaguzi mkuu wa 2022 ni kukiuka Katiba