Habari za Kaunti

Waliohamia ODM juzi waamua kurejea PAA

January 31st, 2024 2 min read

NA ANTHONY KITMO

WANACHAMA wanne wa chama cha kisiasa cha Pamoja Africa Alliance (PAA), wameonekana kuyumbayumba kisiasa baada ya kurudi kwa chama hicho siku chache tu baada ya kupokewa na kinara wa ODM, Raila Odinga jijini Nairobi kama wanachama wapya wa chungwa.

Wanachama hao, Jumanne walitangaza kurudi kwa chama cha PAA huku duru zikisema kuwa wameahidiwa vinono na chama kinachohusishwa na Spika wa Seneti Amason Kingi.

Katika mkahawa mmoja eneo la Nyali, viongozi hao ambao wanaonekana kuwa vigeugeu, walisema waliamua kurudi kwa chama cha PAA baada ya mazungumzo na viongozi wa chama hicho.

“Tulikuwa tumehadaiwa na punde tu tulipokutana na viongozi wa ODM, tuliona heri turudi nyumbani. Hii ni baada ya mazungumzo na Bw Kingi na katibu mkuu Bw Lucas Maitha,” alisema Bw Pascal Makanga, mmoja wa waliorejea kwa PAA.

Baadhi ya waliorejea kwa chama hicho ni pamoja na madiwani wa zamani wa Mwanamwinga Pascal Makanga mwenzake wa Mnarani Daniel Kitsao na aliyegombea kiti cha Junju, Bi Riziki Christine mnamo 2017.

Wakati huo huo, chama cha PAA kilipokea wanachama wawili waliokuwa nyanjani wa ODM ambao ni Bi Victoria Mnyazi, aliyekuwa diwani maalum wa Kilifi na Bw Jonathan Kajwele diwani wa zamani wa Ruruma, Kaunti ya Kilifi.

Katika hafla ya kuwapokea tena viongozi hao, wabunge watatu waliochaguliwa kwa tikiti ya PAA, Bw Gonzi Rai (Kinango), Bw Anthony Kenga Mupe (Rabai) na Tungule Charo ( Ganze), waliapa kuanzisha mchakato mkali ilikuboresha chama hicho nyanjani.
“Chama cha PAA kitakuwa moja ya vyama vikuu siku zijazo na punde tu tutaanzisha usajili wa wanachama wapya kote nchini,” alisema Bw Rai.

Wakati huo huo, vyama hivyo viwili vimweka mikakati kabambe kunyakuwa kiti cha Magarini baada ya mahakama kufutilia mbali uchaguzi wa mbunge wa eneo hilo, Bw Harrison Kombe.

Wiki iliyopita, viongozi wa ODM walipiga kambi eneo la Marafa, ngome kuu ya Bw Kingi, wakisema wako tayari kwa uchaguzi mdogo punde tu Tume ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) itakapotangaza siku ya uchaguzi huo mdogo.

Wakiongozwa na Bw Odinga, viongozi hao walisema eneo hilo litabaki kwa ngome ya ODM licha ya kuwa kijiji cha kinara wa PAA, Bw Kingi.

Hata hivyo, Katibu mkuu wa PAA, Bw Maitha alipuuzilia mbali matamshi ya ODM , akisema kuwa korti ilidhihirisha kuwa chama hicho kina ushawishi mkubwa eneo hilo na Pwani nzima.

“Korti imedhihirisha kuwa PAA ilishinda eneo bunge la Magarini, tunangoja tu kipenga kipigwe turudi uwanjani tuonyeshe ubabe wa PAA,” alisema Bw Maitha.