Habari Mseto

Walioiba bunduki wabambwa

April 3rd, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MAAFISA wa upelelezi wa jinai wamemkamata mwanamume mmoja anayeshukiwa kuwa miongoni mwa majambazi waliovamia kituo cha polisi cha Kibos na kuiba bunduki, risasi kadha na mali nyinginezo.

Kwenye taarifa kupitia akaunti yake ya twitter jana, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema walimkamata mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 19 nyumbani kwake katika kijiji cha Kanyakwar viungani mwa mji wa Kisumu akiwa moja bunduki zilizoibiwa katika kisa hicho mnamo Machi 28, 2020.

“Mshukiwa wa wizi wa kimabavu, mwenye umri wa miaka 19, anayehusishwa na wizi wa silaha kutoka kituo kidogo cha polisi cha Kibos na kisha wizi wa Zaidi ya Sh23,000 kutoka kwa mhudumu wa Mpea katika eneo la Daraja Mbili, Kisumu leo alikamatwa na wapelelezi wa DCI nyumbani kwake katika Kijiji cha Kanyakwar, Kisumu,” DCI ikaandika.

Kulingana na DCI mhudumu wa Mpesa alivamiwa na genge la wanaume watano walikuwa na bunduki aina ya G3 kabla ya kumwibia pesa hizo, simu tatu za mkono na televisheni moja. Kisha walitoroka kwa kutumia pikipiki mbili.

Baada ya tukio hilo maafisa wa upelelezi wa Kisumu wakishirikiana na wenzao kutoka makao makuu ya DCI walianzisha operesheni kali ya kuwasaka washukiwa hao.

Mshukiwa aliyekamatwa jana alipatikana na bunduki moja aina ya G3 nyumbani kwake akiwa ameifunga ndani ya gunia.

“Bunduki hiyo ilitambuliwa kama ile ambayo iliibiwa kutoka kituo cha polisi cha Kibos mnamo Machi 28, 2020 usiku, mvua ikinyesha, watu wasiojulikana walipovunja ghala la silaha na kuiba bunduki tatu, magazine nne na risasi 150,” DCI ikasema.

Iliongeza kuwa baada ya mshukiwa kuhojiwa, aliwaelekeza maafisa hadi nyumba ya mwenzake katika Kijiji hicho hicho.

Katika nyumba hiyo maafisa walipata vitu kadhaa kama vile jaketi tatu za polisi, longi, mishipo, viatu vya maafisa wa usalama, kofia ya polisi na televisheni.

“Vitu hivyo vilitambuliwa kama vile ambavyo viliibiwa kutoka nyumba ya afisa mmoja wa polisi wa cheo cha Inspekta mnamo Machi 10, 2020 alipokwenda Kiganjo kwa mafunzo zaidi, DCI ilisema.

Washukiwa hao wawili wanazuiliwa na polisi huku wapelelezi wakiendelea kuwasaka washukiwa wengine.