Walioingia mitini

Walioingia mitini

WANDERI KAMAU na LEONARD ONYANGO

KUSAMBARATIKA kwa Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI) na sintofahamu kuhusu mwelekeo wa siasa za 2022, imefanya baadhi ya wanasiasa waliokuwa watetezi wa kufa kupona wa vigogo wakuu wa kisiasa nchini, kunyamaza.

Idadi kubwa ya wanasiasa hao walikuwa watetezi sugu wa Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa ODM, Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto.

Wengi wa wanasiasa hao wameingia ‘mafichoni’ katika siku za hivi karibuni na wamekuwa wakikwepa kuandamana na Bw Odinga au Dkt Ruto ambao wameimarisha kampeni zao wakijiandaa kwa kinyang’anyiro cha urais Agosti 9, 2022.

Katika kambi ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, baadhi ya watetezi wao waliofyata midomo ni Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee David Murathe, Mbunge Maalum Maina Kamanda, mwanasiasa Peter Kenneth, wabunge Jared Okello (Nyando), Joshua Kutuny (Cherengany), Alfred Keter (Nandi Hills), Naisula Lesuuda (Samburu Magharibi), Mpuru Aburi (EALA), Peter Kaluma (Homa Bay Mjini), Florence Mutua (Busia) kati ya wengine.

Miongoni mwa waliokuwa watetezi sugu wa Dkt Ruto ambao wameamua kusalia kimya ni Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki, wabunge John Paul Mwirigi (Igembe Kusini), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Khatib Mwashetani (Lungalunga), Vincent Musyoka ‘Kawaya’ (Mwala), Patrick Makau (Mbooni) kati ya wengine.

Baadhi ya wanasiasa pia wameamua kunyamaza baada ya kubaini kwamba viongozi wao wa vyama wana uhusiano wa karibu na wapinzani wao.

Ingawa baadhi yao wanadai “kujishughulisha kuwahudumia wananchi” au kujiendeleza kimasomo, Taifa Jumapili imebaini misimamo ya wengi wao imechochewa na hali ya kutotabirika kwa siasa zinazoendelea nchini.

“Huu ni wakati muhimu sana kwa wanasiasa kufanya uamuzi utakaohakikisha hawajipati kwenye baridi ya kisiasa baada ya uchaguzi mkuu wa 2022. Licha ya kuwa watetezi wa vigogo wakuu wa kisiasa, lazima wahakikishe hawapotezi ushirikiano wao na wananchi,” asema Bw Dismus Mokua, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kimya cha Prof Kindiki hata kuhusu siasa za Kaunti ya Tharaka Nithi kimewakanganya wanasiasa wanaomezea mate kiti cha ugavana.

Seneta Kindiki katika miezi ya hivi karibuni amejitenga na Dkt Ruto na amekuwa akizunguka kutoka kijiji kimoja hadi kingine katika Kaunti ya Tharaka Nithi lakini hajatangaza atawania kiti kipi mwaka 2022.

“Niliamua kurudi nyumbani kutangamana na wenyeji wa Tharaka-Nithi ili kufahamu matatizo yanayowakabili. Baada ya kupokonywa wadhifa wa Naibu Spika wa Seneti, niliamua kurejea nyumbani kutumia muda wangu mwingi kuingiliana na wenyeji,” akasema Prof Kindiki huku akisisitiza kuwa angali anaunga mkono Dkt Ruto.

Kabla ya kimya chake cha ghafla, Bw Murathe ndiye alikuwa akionekana kama ‘sauti’ ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, hasa wakati wa kampeni za kuipigia debe BBI.

Semi zake ziligeuka kuwa ‘utabiri’ wa kisiasa, ambao mara nyingi ulitimia wiki ama siku chache baadaye.

Alikuwa akifanya mahojiano na vyombo tofauti vya habari, huku kauli zake zikiutikisa sana mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao humuunga mkono Dkt Ruto.

Baadhi ya utabiri wake uliotimia ni kufurushwa kwa maseneta sita ‘waasi’ kutoka Chama cha Jubilee (JP).

Bw Murathe pia ‘alitabiri’ kufurushwa kwa mbunge Caleb Kositany (Soy) kama Naibu Katibu Mkuu wa chama.

Alijijengea ushawishi mkubwa kiasi kwamba Dkt Ruto alianza kumtaja moja kwa moja kwenye hotuba zake, kama miongoni mwa watu waliochangia kusambaratika kwa JP.

“Bw Murathe na (Katibu Mkuu) Raphael Tuju ndio sababu kuu za kuvurugika kwa Jubilee,” alidai Dkt Ruto.

Wengine waliojijengea ushawishi huo ni Bw Kamanda. Kabla ya kutupwa kwa BBI na korti, mbunge huyo Maalumu alikuwa akiandamana na Bw Odinga katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo ukanda wa Mlima Kenya, akisisitiza kuwa kinyume na awali, eneo hilo litamuunga mkono kikamilifu kutokana na ushirikiano ambao amempa Rais Kenyatta kupitia kwa handisheki.

Bw Kamanda amewahi kunukuliwa akisema kuwa BBI ndiyo ilikuwa imeweka pamoja Rais Kenyatta na Bw Odinga na kutupwa kwake lilikuwa pigo kubwa.

Mbunge Keter anadai kimya chake kinatokana na hatua yake ya kurejea katika chuo kujiendeleza kimasomo.

“Niliondoka kwenye ulingo wa siasa kwa muda kuangazia masomo yangu. Ninasomea shahada ya uzamili kuhusu Masuala ya Usimamizi wa Biashara (MBA) katika Chuo Kikuu cha Nairobi,” akasema kwenye mahojiano.

Bw Keter, hata hivyo, ameonyesha nia ya kuelekea mrengo wa Dkt Ruto huku akilenga kuwania ugavana wa Nandi.

Mbunge Mwirigi naye anasema kwamba ameamua kurudi nyumbani kuwa karibu na wenyeji, kwani ndio “mabosi wake.”

Wadadisi wa siasa wanasema kuwa wanasiasa wengi walikuwa na matumaini kwamba wangepata nyadhifa mbalimba serikalini endapo BBI ingepita.

“Baada ya BBI kusitishwa na mahakama, wengi waliona kwamba njia ya pekee ambayo wataweza kujiokoa kisiasa ni kurejea walikochaguliwa ili kutopoteza nyadhifa zao. Tutaendelea kushuhudia mwenendo huu kadri uchaguzi unapokaribia,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

You can share this post!

JAMVI: Mtihani mgumu wamsubiri Ruto kuhusu miungano

Nahodha Callum McGregor atia saini mkataba mpya wa miaka...