Habari Mseto

Waliokosa kujiunga na sekondari kuwindwa hadi vijijini

February 8th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

WANAFUNZI wapatao 130,000 bado hawajajiunga na Kidato cha Kwanza licha ya juhudi za serikali kuhakikisha kuwa wanafunzi wote ambao walifanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) 2018 wanajiunga na shule za upili.

Hilo lilibainika Alhamisi kwenye uzinduzi wa kampeni maalum iliyoongozwa na Waziri wa Elimu, Amina Mohamed kuhakikisha wanafunzi hao wamejiunga na shule za sekondari.

Akihutubu kwenye uzinduzi huo jijini Nairobi jana, waziri alisema wanalenga kuwashirikisha maafisa wa utawala, jamaa, wazazi na marafiki wa wanafunzi hao ili kuwashawishi kujiunga na shule za upili.

“Kwa kiwango kikubwa, mkakati wa serikali kutoa hamasisho kwa wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni zimefaulu, lakini hatua zaidi bado zinahitajika kuhakikisha kuwa wote wamejiunga na shule hizo kwa asilimia 100,” akasema.

Jumla ya wanafunzi 1,036,220 walifanya mtihani huo mwaka uliopita. Wanafunzi hao walipangiwa kujiunga na shule za upili kati ya Januri 7 na 18.

Kaunti ya Murang’a ndiyo inayoongoza kwa wanafunzi wengi zaidi waliojiunga na shule za upili.

Hata hivyo, wizara ilieleza kutoridhishwa na idadi chache ya wanafunzi waliojiunga na shule hizo katika kaunti za Mombasa, Lamu, Kwale, Samburu, Isiolo na Tana River.

“Hali hii hairidhishi hata kidogo kulingana na malengo yliyopo. Katika harakati zetu, tutazipa uzito kaunti zilizoandikisha idadi ndogo ya wanafunzi waliojiunga na Kidato cha Kwanza,” akasema Bi Mohamed.

Kwenye kampeni hizo, wizara imendika orodha ya majina ya wanafunzi hao na wanakotoka ili kurahisisha utaratibu wa kuwatambua.

“Hakuna mwanafunzi ambaye ataachwa. Tutashirikiana na wadau wote kama vile maafisa wa utawala ili kuhakikisha kwamba tumewafikia,” akasema.

Kulingana na Mfumo wa Kitaifa wa Kuwasajili Wanafunzi (NEMIS) wanafunzi 640 waliamua kurudia darasa la nane huku 2,299 wakijiunga wa vyuo vya kiufundi

Baadhi ya sababu kuu ambazo zimejitokeza kama vikwazo vikuu ni mimba za mapema miongoni mwa wasichana, ndoa za mapema, ukosefu wa usalama, sababu za kitamaduni na viwango vikubwa vya umaskini hasa katika maeneo kame.

Waziri hata hivyo alisema kwamba wizara yake inapanga kushirikiana na wadau husika kushughulikia changamoto hizo.