Waliokosoa Ruto wapiga magoti

Waliokosoa Ruto wapiga magoti

NA CHARLES WASONGA

WANASIASA wakuu waliomkataa Rais William Ruto kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9 sasa wameamua ‘kumpigia magoti’ na kuelezea nia ya kushirikiana na serikali yake katika nyanja za maendeleo.

Miongoni mwao ni Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli, Gavana wa Kisii, Simba Arati, Naibu Gavana wa Kakamega, Ayub Savula, magavana wa zamani Kivutha Kibwana (Makueni) na James Ongwae (Kisii) na Mbunge wa Tiaty, William Kamket.

Katika siku za hivi karibuni wanasiasa hawa, waliomuunga mkono kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais, wamekuwa wakimtambelea Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi wakiandamana na viongozi kutoka maeneo yao “kujadili masuala ya maendeleo kwa manufaa ya watu wetu”.

Hata hivyo, duru zinasema kuwa ajenda kuu katika mikutano hiyo huwa ni maridhiano ya kisiasa na Rais Ruto, hususan, kwa manufaa ya kibinafsi ya wahusika.

“Wanatumia maendeleo kama kisingizio cha kuhalalisha mikutano yao na Rais Ruto. Ukweli ni kwamba watu hawa kama vile Atwoli na wenzake, wanaenda Ikulu kufanikisha masilahi yao wenyewe wala sio ya jamii yetu ya Waluhya,” Seneta wa Vihiga, Bw Godfrey Osotsi alisema.

Baada ya kukutana na Rais Ruto Alhamisi katika Ikulu ya Nairobi, Bw Atwoli aliweka taarifa fupi katika akaunti yake ya Twitter akisema alijadili masuala ya Shirika la Leba Ulimwenguni (ILO).

“Leo (Alhamisi) asubuhi nilimtembelea Mheshimiwa William Ruto ambapo tulifanya majadiliano kuhusu hatua ya Kenya kuidhinisha mkataba wa ILO C190. Niliomba miadi ya kukutana naye ili kuwasilisha jumbe za makatibu wakuu wa vyama vyote washirika wa COTU,” Bw Atwoli akasema.

Lakini kiongozi huyo wa Cotu aliambatana na wanasiasa wakuu kutoka jamii ya Waluhya kama vile Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Spika wa Bunge Moses Wetang’ula, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale, waziri wa zamani wa Michezo Rashid Echesa na wengine; ishara kwamba ajenda ilikuwa siasa wala sio ILO.

Lakini baadhi ya wanasiasa kutoka Magharibi mwa Kenya walioandamana na Bw Atwoli walisema kiongozi huyo wa COTU ndiye aliyewasilisha maombi ya mkutano huo kwa sababu alitaka kuridhiana na Rais Ruto.

“Bw Atwoli ndiye amekuwa akishinikiza kufanyika kwa mkutano huo kwa sababu alitaka kumwomba msamaha Rais na hilo ndilo lilifanyika,” akasema mwanasiasa huyo aliyeomba tulibane jina lake.

Itakumbukwa kuwa wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, Bw Atwoli alikariri kila mara kwamba Rais Ruto hana nafasi ya kushinda urais.

Alidai kiongozi huyo wa Kenya Kwanza (KKA) angejinyonga baada ya kushindwa Bw Odinga.

Siku moja baada ya Bw Atwoli kutoka Ikulu, ilikuwa zamu ya Bw Arati aliyeongoza ujumbe wa wabunge kutoka eneo la Gusii kuwasilisha matakwa ya maendeleo ya jamii hiyo kwa Rais Ruto.

Gavana Arati amekuwa mshirika wa karibu zaidi wa Bw Odinga, tangu alipohudumu kwa mihula mwili kama Mbunge wa Dagoretti Kaskazini kwa tiketi ya ODM.

Dalili za Gavana Arati kusogea upande wa Rais Ruto zilianza kujitokeza majuma mawili yaliyopita alipowasilisha mchango wa Sh2 milioni kutoka kwa kiongozi huyo wa taifa kwenye hafla ya uzinduzi wa Chama cha Ushirika cha Wahudumu wa Bodaboda katika Kaunti ya Kisii.

Kwa upande wake, Prof Kibwana alitangaza kustaafu siasa Novemba 13, miezi miwili baada ya kugura Azimio na kujiunga na mrengo wa KKA.

Duru zinasema Prof Kibwana ni kati ya viongozi wa Ukambani wanaopigiwa upatu kuteuliwa na Rais Ruto kuwa Mawaziri Wasaidizi (CAS).

Bw Kamket aliye mwanasiasa wa kipekee kutoka Baringo aliyeshinda ubunge kwa tiketi ya chama kilichounga mkono Bw Odinga katika uchaguzi uliopita alisema alijiunga na Kenya Kwanza ili kujiondoa katika “upweke wa kisiasa”.

Wanasiasa wengine wa Azimio wanaoonekana kuegemea upande wa Dkt Ruto ni wabunge Titus Khamala (Lurambi), Emmanuel Wangwe (Navakholo), Benard Shinali (Ikolomani), wote waliochaguliwa kwa tiketi ya ODM. Pia Chris Obure.

  • Tags

You can share this post!

DARUBINI YA WIKI: Toleo Nambari 14 | Desemba 4, 2022

Serikali kuyakagua mahindi yaliyo melini kuhakikisha ni...

T L