Habari Mseto

Waliomlaghai mama Sh40,000 wauawa na umati

December 5th, 2019 1 min read

Na SAMMY KIMATU

[email protected]

WANAUME wawili walioshukiwa kumlaghai mwanamke Sh40,000 walipigwa na kuuawa na umma baada ya mwanamke mlalamishi kupiga kamsa.

Tukio hilo la nyakati za jioni lilitokea katika barabara ya Haile Selassie katika Kaunti wakati wahusika walikuwa wakicheza kamari.

Wananchi waliitikia haraka na kuwakanata wawili hao na kuwapiga mithili ya mbwa msikitini, na kufariki papo hapo.

Wenzao waiponea kifo kwa tundu la sindano baada ya kufanikiwa kutoroka wakielekea pande tofauti.

Inadaiwa washukiwa waliendesha kamari wakiwaahidi washiriki tuzo baada ya mmoja kuchukua “nambari za kushinda bahati.”

Wananchi walishtumu polisi na maafisa wa Kaunti ya Nairobi kwa kushirikiana na walanguzi katikati ya jiji.

Katika eneo la tukio, mwandishi wetu alipata vipande vya fanicha za plastiki na mawe karibu na miili.

Pia kulikuwepo pikipiki bila nambari za usajili, na sanduku tupu za vifaa vya kielektroniki na bidhaa zingine zinazotumika kuwavutia wapita njia.

Makundi ya wanaochezesha karata mitaani hufanya kazi katika vikundi vya watu zaidi ya 10 wakiwemo wanaume na wanawake.

Washukiwa hao hupatikana karibu na kituo cha mabasi cha Bus Station, kando ya barabara za Ladhies (Karibu na ukuta wa Soko la Muthurwa), mzunguko wa barabara ya Pumwani (karibu na taa za trafiki), karibu na Jengo la Athusi, kwenye barabara ya Temple Road na Salvation Army.

Mlalamishi alipohojiwa alisema anaishi eneo la Mwiki, Kasarani na alirudishiwa Sh10,000 washukiwa walipoona kitumbua chao kimeingia mchanga.