Habari

Waliompa ajuza wa miaka 83 bangi wasakwa

February 6th, 2019 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

POLISI katika Kaunti ya Murang’a wanawasaka vijana watatu wanaodaiwa kumlazimisha nyanya wa miaka 83 avute bangi alipowakanya wakome kutumia shamba lake kujificha wanapovuta bangi.

Ajuza huyo alipagawa baada ya kuvuta bangi hiyo na ikabidi anyweshwe maziwa ili makali ya bangi hiyo yashuke kabla ya kukimbizwa hospitalini.

Vijana hao wanaofahamika vyema na majirani wana umri wa kati ya miaka 17 na 21.

“Baada ya vijana hao kununua bangi hiyo, waliingia katika boma la ajuza huyo mwendo wa saa tatu usiku na wakamlazimisha kuvuta msokoto mmoja. Kuna habari kuwa ajuza huyo alikuwa amewaonya dhidi ya kutumia shamba lake kuvuta bangi hiyo na ndiposa kwa hasira wakaamua kumwadhibu,” alisema mkuu wa polisi wa utawala eneo hilo, Bw James Limo.

Kwa kuwa boma la ajuza huyo liko karibu na barabara, wapita njia walimsikia akibishana na vijana hao katika kijiji cha Kianda, Kaunti ndogo ya Kigumo ndiposa wakamnusuru.

Ajuza huyo alipelekwa katika hospitali kuu ya Maragua ambapo alitibiwa kwa kile wauguzi walitaja kuwa athari za ulevi wa bangi kupindukia.

Bw Limo alisema maafisa wanawasaka vijana hao watatu pamoja na mlanguzi wa bangi, ambao walitoweka baada ya kisa hicho.

Alisema kuwa tayari ajuza huyo amerekodi taarifa rasmi kuhusu tukio hilo.

Mwenyekiti wa mpango wa Usalama wa Nyumba Kumi eneo hilo, Bw James Kimani, alisema muuzaji bangi anayesakwa amekuwa katika biashara hiyo kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

Chifu wa eneo hilo, David Ng’ang’a alithibitisha kuwa kuna habari kuhusu mlanguzi huyo wa bangi: “Ni ukweli kuwa kuna kijana ambaye huuza bangi katika eneo hili. Tumemkamata mara kadhaa lakini haonekani kurekebisha mienendo yake. Kisa hiki dhidi ya nyanya kimemweka katika darubini ya usalama na ni lazima sasa biashara yake ivunjwe,” akasema.

Alisema kuwa hana habari kuwa mlanguzi huyo amekuwa akihonga maafisa wa usalama kwa Sh1,000 kila Ijumaa ili kukwepa kutiwa mbaroni.