Waliomuua msichana 9, wakimtoa mapepo wakamatwa

Waliomuua msichana 9, wakimtoa mapepo wakamatwa

NA MARY WANGARI

DELGODA, Sri Lanka

POLISI nchini Sri Lanka walisema Jumanne, Machi 2, 2021, kuwa wamewakamata watu wawili kuhusiana na mauaji ya msichana mwenye umri wa miaka 9.

Mtoto huyo alitandikwa mara kadhaa wakati wa tambiko waliloamini lingewafukuza mapepo.

Washukiwa wawili – mwanamke aliyekuwa akifanya tambiko la kufukuza mapepo na mamake msichana huyo walifikishwa kortini mnamo Jumatatu, Machi 2, 2021.

Walisomewa mashtaka kuhusu kifo cha msichana huyo kilichotokea Delgoda, mji mdogo wa takriban kilomita 40 Kaskazini Mashariki mwa jiji kuu la Colombo.

Mahakama iliamrisha washukiwa hao kuzuiliwa hadi Machi 12

Kulingana na msemaji wa polisi Ajith Rohana, mamake mtoto huyo aliamini kuwa bintiye alikuwa amepagawa na mapepo na kumpeleka nyumbani kwa mpiga ramli ili afanyiwe tambiko la kumtoa mashetani.

Rohana alisema mpiga ramli huyo kwanza alimmiminia mafuta mtoto huyo kisha akaanza kumgonga mara kadhaa kwa kutumia kiboko.

Msichana huyo alipopoteza fahamu, alipelekwa hospitalini ambapo aliaga dunia.

“Mwanamke aliyemfanyia tambiko msichana huyo anafahamika eneo hilo kwa kutoa huduma kama hizo katika miezi ya hivi karibuni na polisi wanachunguza iwapo kuna mtu mwingine yeyote aliyedhulumiwa,” alisema Rohana.

Aidha, msemaji wa polisi alihimiza umma kujihadhari kuhusu huduma kama hizo kwa kuwa msichana huyo si wa kwanza kutokana na tambiko kama hilo.

You can share this post!

Makamu wa Rais Zimbabwe ajiuzulu kuhusu video ya ngono

Taharuki kuhusu teknolojia ya kutambulisha nyuso