Habari Mseto

Waliomuua mwanahabari wa The Star kushtakiwa

November 25th, 2019 2 min read

Na DICKENS WASONGA

WATU watano ambao wamekuwa wakizuiliwa na maafisa wa polisi wa Siaya kuhusiana na kifo tata cha mwanahabari wa gazeti la The Star Erick Oloo Alhamisi, wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu.

Kulingana na afisa wa cheo cha inspekta anayefanya uchunguzi huo Tobias Akumu, washukiwa hao hawatatakiwa kujibu mashtaka na badala yake polisi wataomba muda zaidi kuwazuilia ili kukamilisha uchunguzi wao.

Washukiwa wanne kati yao walikamatwa siku ambayo mwili wa Bw Oloo ulipatikana kwenye nyumba ya afisa wa cheo cha inspekta kwa jina Sabina Kerubo wiki jana.

Wengine ambao walikamatwa pamoja na Bi Kerubo ni mjakazi wake Joyce Awuor, mwanawe ambaye hajafikisha umri wa miaka 18 na mpenzi wa afisa huyo kwa jina Victor Ogola Luta.

Mnamo Ijumaa jioni, makachero wakiongozwa na DCIO wa Ugunja Andrew Nyambachi walikamata mshukiwa wa tano ambaye anatambulika kama Franklin Ogola Luta (nduguye Victor) kwenye maficho yake katika kijiji cha Mutumbu, Yala.

Bw Oloo anadaiwa alivamiwa kwenye nyumba ya afisa huyo Jumatano jioni huku washukiwa watano wote ikithibitishwa walikwepo wakati wa kisa hicho.

Taifa Leo pia imebaini kwamba Mamlaka Huru ya Utendakazi wa Polisi (IPOA) imeanzisha uchunguzi kuhusiana na kuhusishwa kwa Bi Kerubo kwenye mauaji ya mwanahabari huyo ambaye alikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi naye kwa muda wa miaka miwili.

Duru zinaarifu kwamba maafisa watatu kutoka afisi za IPOA jijini Kisumu walitembelea kituo cha polisi cha Ugunja Ijumaa wiki jana kuanzisha uchunguzi.

Kikosi hicho cha IPOA kikiongozwa na Inspekta Mkuu Geoffrey Aramis walitembelea nyumba ya Bi Kerubo ambaye sasa limezingirwa kama eneo la mauaji.

Maafisa hao watamhoji polisi huyo kisha kuangalia faili inayojumuisha taarifa za uchunguzi unaoendeshwa na DCI kulingana na duru kutoka kwa IPOA.

Mnamo Jumapili Mkurugenzi wa Mawasiliano wa IPOA Dennis Oketch alithibitisha kwamba uchunguzi kuhusu kisa hicho unaendelea.

Haya yanajiri huku ripoti ya uchunguzi wa postmortem iliyotolewa Jumamosi ikifichua kwamba marehemu aliaga dunia baada ya kugongwa kichwani na kifaa butu.