Habari Mseto

Waliomuua Sharon Otieno wakamatwe mara moja – Raila

September 6th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga amekashifu mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo Sharon Otieno ambaye aliangamizwa kinyama akiwa mja mzito, akitaka waliohusika kukamatwa na kufungwa kwa haraka.

Bw Odinga alisema chama cha ODM kinaungana na Wakenya kukemea kitendo cha aina hiyo, ambacho kilimwacha mwanafunzi kuuawa kwa njia ya kihayawani.

“Tunatumai kuwa waliohusika katika kitendo hiki cha kinyama watakamatwa haraka iwezekanavyo. Tunataka kuona wakikamatwa na kufungwa,” akasema Bw Odinga.

Aidha, katika kikao hicho cha Jumatano, Bw Odinga aliwataka waliokuwepo kusimama kwa dakika moja kama ishara ya heshima kwa Bi Otieno, ambaye alisema hakupaswa kupokea kifo cha aina hiyo.

Semi zake zilikuja saa chache baada ya viongozi wengine kutoka eneo la nyanza kukemea kitendo hicho, wakitaka mhusika mkuu wa mauaji hayo kukamatwa.

“Hatutaki kusikia watu wadogowadogo wakikamatwa tu, tunataka mhusika mkuu hata kama ni mbunge ama gavana kama tunavyosikia. Msichana huyu alikuwa mja mzito na alikuwa akipata elimu kuboresha maisha yake na ya wazazi wake,” akasema mwakilishi wa wanawake kaunti ya Homa Bay, Bi Gladys Wanga.