Waliong’aa KCSE wasimulia madhila waliyopitia

Waliong’aa KCSE wasimulia madhila waliyopitia

GEORGE ODIWUOR, SHABAN MAKOKHA, EVANS KIPKURA na MANASE OTSIALO

BAADHI ya wanafunzi waliong’aa kwenye mtihani wa KCSE mwaka jana walivumilia matatizo tele ikiwemo kutumia choo kusoma na vitisho vya usalama.

Mwanafunzi bora wa pili nchini kwenye mtihani huo Alan Wasonga alivumilia matatizo tele mtaani Kibera na kulazimika kuingia chooni kusoma shule zilipofungwa kwa sababu ya janga la corona.

Aidha kutokana na umaskini mkubwa wa familia yake, Wasonga aliyekuwa akisomea shule ya upili ya Agoro Sare alilazimika kulala kwenye kochi kila usiku.

Japo alikuwa akipata muda mzuri wa kusoma akiwa shuleni, mtaani Kibera alilazimika kuhepa na kusoma kwa kuingia chooni kwa kuwa mamake hakutaka taa iwe ikiwaka wakati wenzake walikuwa wamelala.

“Mimi ni mshonaji nguo Kibera na wakati mwingine huwa ninafika nyumbani saa nne usiku nikiwa na uchovu mwingi. Baada ya kuwapikia huwa naenda kulala hadi siku inayofuatia,” akasema Bi Oloo.

Mwanafunzi mwengine aliyeng’aa katika KCPE ni Brian Peter kutoka Kaunti ya Vihiga nusra asijiunge na shule ya upili kutokana na ukosefu wa karo.

Bw Peter ambaye aliibuka wa kwanza katika shule ya wavulana ya Hobunaka na wa pili katika kaunti hiyo, alisema kuwa japo mwanzoni aliitwa katika shule ya upili ya Shimo la Tewa, alikosa kujiunga nayo kwa sababu ya ukosefu wa karo.

Licha ya kutoka shule isiyofahamika, mwanafunzi huyo alipata alama A ya alama 82. Babake Livingstone Omuhindi alifichua kuwa usimamizi wa shule hiyo uliafikia uamuzi wa kumsaidia kwa kufuta karo ya shule aliyodaiwa.

Katika Kaunti ya Kakamega, Collins Otema ambaye aliacha masomo na kurejea shuleni kwa muhula wa tatu alishangaza kwa kupata alama ya B+ ya alama 64 . Bw Otema alikuwa akisoma katika Shule ya Upili ya St Joseph Shibale.

Naye wanafunzi bora wa kike katika Kaunti ya Mandera Rahma Ibrein amesema kwamba kung’aa kwake kunatokana na bidii licha ya kukosa shule mara kadhaa kutokana na ukosefu wa usalama.

Bi Rahma alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Takaba na alisema kuwa walikuwa wakikabiliwa na uhaba wa walimu lakini akawajibika kwa kutia bidii na kufuzu vyema katika mtihani wake. Alipata alama ya B+ katika mtihani huo.

“Kupata alama kama hizi katika kaunti ya Mandera si jambo rahisi. Hatuna walimu wa kutosha katika shule na mazingira ya masomo huwa hayaridhishi kama maeneo mengine nchini,” akasema.

Bi Rahma alifichua kwamba aliamua kutia bidii kwa kushirikiana na wanafunzi wengine kutoka shule ambazo huwa zina utulivu wakati wa mtihani.

“Nimekuwa nikiomba na wazazi wangu walinipa motisha unaohitajika ili kung’aa kwenye masomo yangu. Bidii na subira tena imani kwa mwenyezi mungu zimenisaidia,” akaongeza.

Aidha, wanafunzi kutoka shule zinazopatikana katika kaunti za Elgeyo Marakwet na West Pokot walifanya vizuri katika mtihani wao licha ya kaunti hizo mbili kukabiliwa na utovu wa usalama.

Baadhi ya shule hizo ni Tot, St Augustine Kapyego na Kamalei ambapo wanafunzi walisitisha masomo yao kwa siku kadhaa kutokana na uvamizi wa majangili.

You can share this post!

Kenya yasitisha safari za ndege Somalia

Waibuka wa kwanza Nyeri licha ya kuwa ni zeruzeru