Habari Mseto

Waliong'olewa paa kwa kukosa kulipa kodi wapata ufadhili

May 3rd, 2020 1 min read

MISHI GONGO na WINNIE ATIENO

FAMILIA nne zilizoachwa bila makao baada ya mmiliki wa nyumba kung’oa paa kwa kukosa kulipa kodi wamepata sababu ya kutabasamu baada ya watu wenye huruma na uwezo vilevile kuwatafutia makao mapya.

Wafadhili hao walijtokeza na kusaidia familia hizo kwa kuwatafutia makazi mapya na kuwalipia kodi ya miezi miwili kisha kuwanunulia chakula, baada ya kisa chao kuangaziwa na ‘Taifa Leo’ siku chache zilizopita.

Mmoja wa wahasiriwa wa tukio hilo, Bi Ruth Omumia, 38, na mumewe Joseph Omumia, wamewashukuru watu hao kwa ufadhili waliopata kutoka kwao.

“Nawashukuru nyote mliojitokeza kutusaidia; Mungu awabariki,” akasema Bi Omumia.

Wafadhili akiwemo mtetezi wa haki za kibinadamu Bw Mathias Shipeta alisema waliungana na wafadhili wengi ili kuwasaidia wahasiriwa baada ya kuona masaibu yao yameangaziwa mtandaoni na katika gazeti.

“Tuliwanunulia chakula na kuwalipia kodi ya miezi miwili kama njia ya kuwapunguzia mzigo wa maisha,” akasema Bw Shipeta.

Bw Omumia ni mmoja wa zaidi ya vibarua 100 walioachishwa kazi kutoka kwa kiwanda cha utengezaji na kusafirisha bidhaa (Export Processing Zone) kilichoko Changamwe kufuatia athari za janga la corona.

Wawili hao waliokodi chumba kimoja, wanatakiwa kulipa kodi ya Sh3,000 kila mwezi.

“Aprili 20, 2020, mwenye nyumba alikuja kudai kodi ambapo tulimsihi kutupa muda zaidi wa kulipa lakini alikataa. Tuliambiwa tulipe ama tutoke kwa nyumba yake. Tarahe 27 akatuma watu kuja kung’oa milango na mabati,” akasema Bi Omumia.

Mwanamke huyo alisema wanadaiwa kodi ya miezi mitatu.

Bi Omumia na mumewe sasa wamelazimika kuwapeleka watoto wao wawili kuishi na mwalimu wao.

Aidha Bi Omumia amesema japo walimuomba mwenye nyumba achukue pikipiki ya mumewe hadi pale wangepata uwezo wa kulipa deni lao, alikataa.

“Hatuna pahala pa kwenda na tunaomba wahisani kutusaidia kwani tangu kutolewa mabati tumekuwa tukinyeshewa,” akasema wakati huo.

Wawili hao wamesema waliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Mikindani.