Walionufaika na kupoteza kwa uamuzi wa korti kuhusu BBI

Walionufaika na kupoteza kwa uamuzi wa korti kuhusu BBI

Na Cecil Odongo

BAADA ya Mahakama ya Rufaa kukubaliana na uamuzi wa mahakama kuu wa kuzima mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) Ijumaa, kuna wanasiasa ambao wamenufaika na uamuzi huo huku wengine wakionekana kupata pigo.

Wafuasi wa Naibu Rais Dkt William Ruto na viongozi wanaounga azma yake walikesha mitandaoni na kushabikia kile walichotaja kama ushindi dhidi ya mrengo wa ‘handisheki’.

Dkt Ruto amekuwa akiongoza kampeni ya kupinga marekebisho hayo ya katiba kupitia BBI, na uamuzi wa korti unaonekana kumpa nguvu kuelekea 2022.

“Mungu amewaokoa Wakenya kutoka muungano wa watu wenye mamlaka zaidi waliokuwa wakilenga kuharibu katiba yetu. Mungu wetu amewasaidia mahasla, wasiokuwa na kazi na wakulima wanaohangaika kuanza kuboresha uchumi wetu kupitia mfumo wa ‘bottom up’,” akaandika Dkt Ruto.

Aidha, madiwani ni kati ya walionufaika wakati wa mchakato mzima wa BBI kwa kuruhusiwa kuchukua Sh2 milioni kama mkopo wa kununua magari. Hii ilikuwa njia ya kuwashawishi waipitishe BBI kwenye mabunge ya kaunti zao.

Vilevile wanakamati 14 na wanajopo wa BBI walivuna vinono kwa kulipwa marupurupu makubwa kutokana na vikao walivyoviandaa katika kaunti zote 47.

Rais Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga wanaonekana kupotezazaidi kutokana na uamuzi wa mahakama.

Wawili hao wamekuwa mstari wa mbele kurindima ngoma ya BBI katika ziara zao mbalimbali nchini.Hata hivyo, ni Bw Odinga ambaye anaonekana kupata pigo zaidi, ikizingatiwa analenga kuwania kiti cha urais kwa mara ya tano.

Ikizingatiwa sasa hakuna nyadhifa za ziada zilizopendekezwa kwenye BBI, Bw Odinga ana kibarua kigumu kuwaridhisha wanasiasa wote watakaounga azma yake hasa kumteua mwaniaji mwenza.

Ingawa hivyo, Bw Odinga alionekana kutabiri hilo mapema na wiki jana akawaambia wafuasi wake kuwa hana nia ya kukata rufaa iwapo BBI itaangushwa kortini.

Waziri huyo mkuu wa zamani ameanza kujijenga upya kwa kuandaa makongamano ya kujivumisha kwa raia.Hali ni hiyo hiyo kwa viongozi wa OKA ambao walikuwa wakisubiri uamuzi kuhusu BBI kabla ya kuamua mustakabali wao wa kisiasa.

Vigogo hao Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya), Musalia Mudavadi (ANC) na Gideon Moi wa Kanu sasa watalazimika kurejea mezani na kuamua mpeperushaji bendera wa muungano wao na mwaniaji mwenza.

You can share this post!

Mwanamume na wanafunzi wawili waangamia kisimani

Wadau wateta kampuni ya Joho kupewa kandarasi