Habari Mseto

Waliopatikana na simu ya polisi aliyetoweka watupwa ndani

April 17th, 2020 1 min read

Na Richard Munguti

Raia wawili wa Uganda Sharif Wanabwa na Martin Wasike pamoja na Mkenya Phoebe Anindo Andayi wamezuiliwa kwa siku 30 kueleza aliko afisa wa polisi Abel Misati aliyetoweka Januari 21 2020.

Misati alikuwa akihudumu katika kituo cha polisi cha Kamukunji na alikuwa na cheo cha konstebo.

Watatu hao waliagizwa wazuiliwe na hakimu mwandamizi Bernard Ochoi.

Akiwasilisha ombi la kuzuiliwa kwa washukiwa hao Koplo Nathan Amboga alisema watatu hao walikutwa na simu ya afisa huyo wa polisi.

“Konstebo Misati alitoweka Januari 21 mwaka huu,” akasema kiongozi wa mashtaka Bw Ombaga.

Misati alikuwa amepewa likizo ya siku mbili January 19/20 2020 lakini hakurudi kazini.

Afisa anayesimamia nyumba za maofisa katika kituo cha polisi Ibrahim Molu alimpigia simu Misati lakini haikuchukuliwa.

Uchunguzi uliofanywa ulibaini simu ya Misati ilitumiwa na watatu hao. Mahakama ilifahamishwa kwamba Misati hajulikani aliko.

Hakimu alielezwa washukiwa hao watatoroka ikiwa wataachiliwa.

Bw Ochoi alielezwa kuwa mshukiwa mwingine Sam Wareke anayetuhumiwa alishirikiana na washukiwa alitorokea Uganda.

Hakimu aliamuru washukiwa wazuiliwe hadi Mei 11 2020.