Habari Mseto

Waliopiga mawe ndege ya Raila wakati wa kampeni 2022 wana kesi ya kujibu – Hakimu

January 13th, 2024 1 min read

NA TITUS OMUNDE

MFANYABIASHARA na mkulima mmoja kutoka Eldoret ambao wanakabiliwa na mashtaka ya kupiga mawe helikopta iliyombeba kiongozi wa ODM Raila Odinga, jana walipatikana na kesi ya kujibu katika mahakama ya Eldoret.

Hakimu Mkuu Mwandamizi, Bw Mogire Onkoba, aliwapata Abednego Kiptanui Kemboi na Kenneth Kipkogei Sawe na kesi ya kujibu kuhusiana na uharibifu wa mali baada kuharibu ndege na kusababisha fujo kwa njia ambayo ingeweza kusababisha ukosefu wa amani.

Wawili hao wanadaiwa kuvamia helikopta hiyo mnamo Aprili 1, 2022 wakati wa mazishi ya marehemu Jackson Kibor katika eneo la Kabenes kaunti ndogo ya Soy.

Kulingana na mashtaka, wawili hao pamoja na wengine ambao hawakufikishwa mahakamani wakiwa katika shamba la marehemu Kibor, kinyume cha sheria walisababisha uharibifu wa helikopta aina ya Euro-5Y-DSB kwenye kioo cha mbele na kioo cha upande wa kulia chenye thamani ya Sh577 ,500 mali ya kampuni ya Youth Limited.

Pia walituhumiwa kwa kuhatarisha usalama wa abiria na ndege iliyokuwa ikipaa. Wawili hao walipofikishwa kortini kwa mara ya kwanza Aprili 27, 2022, walikanusha shtaka hilo pamoja na mashtaka mawili mbadala. Waliachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 na mdhamini wa kiasi hicho.

Wawili hao kupitia kwa wakili wao Bw George Sonkule , waliambia mahakama nia yao ya kuwasilisha mahakamani mashahidi 20 . Tayari mashahidi 14 wametoa ushahidi.

Jana, wakili Sonkule aliiambia mahakama anakusudia kuwasilisha mashahidi waliosalia . Mahakama iliamuru waendelee kujitetea Januari 24.