Siasa

Waliopinga hoja ya kumvua wadhifa Kindiki kuangukiwa na shoka

May 24th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MASENETA wanne kati ya saba ambao waliopinga hoja wa kumng’oa mamlakani Seneta Kithure Kindiki kutoka wadhifa wa Naibu Spika sasa watapokonywa nyadhifa zao za uongozi katika kamati za seneti.

Kiranja wa wengi Irungu Kang’ata alisema adhabu hiyo itawafika maseneta Samson Cherargei (Nandi), Aaron Cheruiyot (Kericho), Andrew Lang’at (Bomet) na John Kinyua (Laikipia) kwa kupiga kura ya LA kwa hoja hiyo kinyume na msimamo wa Jubilee.

Hii ina maana kuwa Bw Cherargei atapoteza wadhifa anaoshikilia wa Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Haki, Sheria na Haki za Kibinadamu huku Bw Lang’at akivuliwa wadhifa wa mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Elimu.

Bw Kinyua atapoteza cheo cha Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi huku Bw Cheruiyot akikabiliwa na hatari ya kupokonywa nafasi, yenye hadhi kuu, ya Kamishna wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC).

“Mojawapo ya wajibu wangu kama kiranja wa wengi ni kufanya mabadiliko katika uanachama wa Jubilee katika kamati za Seneti. Kuanzia Jumatatu nitaanza shughuli ya kufanya mabadiliko katika kamati hizo kwa kuwaondoa maseneta ambao walikiuka msimamo wa chama kwa kupinga hoja hiyo,” akasema.

Bw Kang’ata, kwenye taarifa, alieleza kuwa kabla ya kujadiliwa kwa hoja hiyo aliwatumia ujumbe maseneta wote 38 wa Jubilee akiwataka kuiunga mkono “kwa sababu chama kimepoteza imani na Profesa Kindiki.”

Maseneta wengine wa Jubilee waliopinga hoja iliyopitishwa katika kikao maalum Ijumaa wiki jana, ni Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Susan Kihika (Nakuru) na Profesa Kindiki mwenyewe.

Tayari watatu hawa wameadhibiwa kwa kuvuliwa nyadhifa walizoshikilia za Kiongozi wa Wengi, Kiranja wa Wengi na Naibu Spika, mtawalia

Na ingawa Seneta wa Meru Mithika Linturi alilaani hoja hiyo na kusisitiza kutoiunga mkono, alikwepa shughuli ya upigaji kura kwa kuondoka ukumbini baada ya kukamilika kwa mjadala.

Jumla ya maseneta 54 wa Jubilee na upinzani walipiga kura ya NDIYO kwa hoja ambayo mwanzoni ilichochea malumbano makali kati ya Bw Murkomen na Kiongozi wa Wachache James Orengo.

Na maseneta Moses Wetang’ula (Bungoma, Ford Kenya), Beth Mugo (Seneta Maalum, Jubilee) na Seneta wa Embu (Jubilee) ambao hawakuhudhuria kikao hicho, pia walipiga kura ya NDIYO.

Maseneta watano wa Jubilee wanaokabiliwa na tishio la kufurushwa chamani kwa kukwepa mkutano wa kundi la maseneta wa mrengo huo katika Ikulu, pia walibadili msimamo na kuunga kuondolewa kwa Profesa Kindiki.

Wao ni Millicent Omanga, Falhada Dekow, Naomi Waqo, Victor Prengei na Mary Seneta; wote wakiwa maseneta maalum.