Michezo

Waliosema Oliech amezeeka waombe radhi – Mashabiki

January 10th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa Gor Mahia wamewataka waliotilia shaka uwezo wa mshambuliaji Dennis “The Menace” Oliech kusakata soka na kuchana nyavu waombe msamaha.

Wakitoa maoni yao baada ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 33 kufungia mabingwa watetezi Gor bao la ushindi wakichapa Posta Rangers 2-1 Jumatano, wanasema Oliech alikuwa sajili ya busara na anastahili mshahara wa Sh350, 000 ambao atalipwa kila mwezi katika kandarasi yake ya miaka miwili aliyosaini Januari 2, 2019.

Shabiki Michael Nyapoya anasema, “The Menace….Pongezi…mashabiki kadhaa walikutilia shaka ulipoajiriwa na K’Ogalo na wakasema Gor iliharibu fedha kukusajili. Tafadhali mashabiki mliotoa matamshi haya, mezeni maneno yenu na muombe msamaha…Oliech aishi milele!”

Naye Blax Lichman anasema, “Oliech yuko sawa; anastahili kulipwa Sh350, 000 kila wiki.”

“Kama Menace anachukua mechi mbili kupata bao katika kipindi cha kwanza, basi atahitaji mechi ngapi kupachika mabao 20 msimu huu. Hongera Deno,” anasema Alfred Ndege.

Oliech amerejea katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) baada ya miaka 15. Baada ya kuondoka Mathare United mwaka 2003, alizunguka mataifa ya Qatar, Ufaransa na Milki za Kiarabu kwa soka ya malipo kabla ya kutua Gor. Mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Mathare United mnamo Januari 6 ambayo ilitamatika 1-1. Aliingia mechi hiyo kama mchezaji wa akiba kabla ya kuanzishwa na kocha Hassan Oktay dhidi ya Rangers.