Walioshindwa ugavana Kwale waungana kuwasilisha kesi mahakamani

Walioshindwa ugavana Kwale waungana kuwasilisha kesi mahakamani

NA SIAGO CECE

WAGOMBEAJI watatu wa ugavana walioshindwa katika Kaunti ya Kwale, wameungana kwa nia ya kwenda mahakamani kupinga ushindi wa Bi Fatuma Achani.

Aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Kilimo, Prof Hamadi Boga (ODM), Mwenyekiti wa Kitaifa wa Wiper, Bw Chirau Ali Mwakere, na Bw Chai Lung’anzi (PAA), wamepinga matokeo yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Wanadai kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na dosari nyingi, jambo ambalo halipaswi kupuuzwa ili kuwanyima wakazi wa Kwale haki ya kuchagua viongozi wao.

Prof Boga alisema yuko tayari kwenda mahakamani kwa kuwa amekosa imani na matokeo ya IEBC, akidai alishuhudia makosa mengi yaliyofanyika wakati wa uchaguzi huo.

“Tuliona makosa mengi kwa vituo vyote vinne vya kuhesabu kura. Kulikuwa pia na utumizi haramu wa vifaa vya kupiga kura kwa vituo hata baada ya muda wa uchaguzi kuisha,” Prof Boga alisema.

Kwa upande wake, Bw Tsawe Munga, ambaye alimwakilisha Bw Mwakwere, alisema hawatakubali matokeo ya kulazimishiwa kiongozi.

“Ni makosa kwa viongozi kupewa cheti ilhali hawakuchaguliwa. Tutapeleka swala hili mahakamani na tuna imani kwamba uchaguzi utarudiwa katika kaunti hii ili kila mkazi awe na haki ya kuchagua kiongozi wake,” Bw Munga alisema.

Bw Lung’anzi alidai kuwa, juhudi zao za kuwasilisha malalamishi kwa IEBC kabla matokeo kutangazwa, ziliambulia patupu.

Alikuwa ameandamana na mwaniaji kiti cha useneta, Bw Mudzo Nzili, miongoni mwa wanasiasa wengine wenye malalamishi.

“Hatuna imani na tume hiyo. Mambo mengi yaliyotokea yamewanyima wakazi wengi wa Kwale haki zao. Tuliona hitilafu nyingi katika mchakato mzima wa uchaguzi,” Bw Lung’anzi alisema.

Bw Nzili alisema wawaniaji hao watakuwa wakielekea mahakamani kutafuta haki.

“Tunataka wakazi wa Kwale wapewe nafasi ya kuwachagua viongozi wao. Tunaelekea mahakamani na tunatumai kuwa kutakuwa na uchaguzi tena ili wakazi wengi wa Kwale wapate kiongozi wanayemtaka,” akasema.

Aliongeza kuwa hawapingi uchaguzi wa mtu yeyote, bali wanapinga mchakato mzima ambao wanahisi ulikuwa na mapungufu mengi.

Malalamiko hayo yanakuja baada ya IEBC kutangaza washindi katika nyadhifa za useneta, mwakilishi wa kikena ugavana katika Kaunti ya Kwale.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge wa zamani afaulu udiwani Wadi ya Jaribuni

Usalama waimarishwa taifa likisubiri matokeo ya kura za...

T L