Habari Mseto

Waliosomea Starehe Girls kukwea vilima kufadhili elimu ya watoto maskini

June 25th, 2019 2 min read

NA MWANDISHI WETU

SHULE ya Upili ya Wasichana ya Starehe, Nairobi mwaka huu inasherehekea miaka sitini tangu kuasisiwa kwake na mipango kadha imetayarishwa na waliosomea shuleni humo kuchangisha fedha za kufadhili elimu ya watoto kutoka familia duni nchini. 

Mojawapo ya mipango hiyo ni kuvikwea vilima vya Lodwar katika Kaunti ya Turkana pamoja na Mlima Kenya, huku wanaoshiriki wakiwaomba marafiki kuwasaidia kwa mchango wa kifedha.

Mojawapo ya wanafunzi waliopokea elimu bila malipo katika shule hiyo Bi Assumptah Wausi (pichani) Jumanne aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa atawaongoza wenzake kutoka Kaunti ya Turkana kuvikwea vilima vya Lodwar hapo Juni 30.

“Lengo kuu ni kuchangisha zaidi ya Sh1 milioni kufadhili elimu ya sekondari ya wasichana na wavulana watakaoitwa kujiunga na Starehe Girls au Starehe Boys,” akasema.

“Starehe ilitunza, ikanilea na kunisomesha. Mbegu iliyopandwa ndani yangu ya elimu imemea na kuzaa matunda ambayo yameniwezesha kusomesha ndugu zangu na kusaidia wazazi,” akaongeza.

Akisomea katika Shule ya Msingi ya Wautu, Kaunti ya Makueni, Bi Wausi alizoa alama 417 mnano mwaka  2005 katika mtihani wa Darasa la Nane KCPE. Alipata ufadhili wa shule ya kitaifa ya Starehe Girls kwa sababu wazazi wake hawakuwa na uwezo kifedha kumwelimisha.

“Nilijiunga na Starehe Girls hapo 2006 na kumaliza kidato cha nne mwaka wa 2009. Baadaye nijiunga na Chuo kikuu cha Moi na kuhitimu mwaka 2015. Niliajiriwa na FSD Kenya kisha nikafanya kazi na benki ya Equity,” akasema huku akitabasamu.

Shule ya upili ya Starehe Boys Centre ambayo baadaye ilipanuka na kujenga Stareeh Girls ilianzishwa na hayati Dkt Geoffrey Griffin pamoja na wengine mwaka wa 1959.

Lengo kuu la kuanzisha lilikuwa kuwasaidia mayatima na watoto wa mtaani wakati kucha za ukoloni zilikuwa zimeathiri familia nyingi Kenya.

Kwa miaka 60 tangu Starehe ianzishwe, imekuza na kulea maelfu ya wanafunzi ambao wameng’aa katika nyanja tofauti nchini. Maisha ya familia nyingi Kenya yamebadilishwa kupitia juhudi zake Dkt Griffin kwa kupanda mbegu ya elimu. Mwaka wa 2005 Starehe Girls ilianzishwa na kufuata nyayo za shule ya wavulana ya Starehe boys.

Dkt Griffin alizaliwa mwaka wa 1933 mjini Eldoret. Alijiunga na shule ya Prince of Wales iliyobadilishwa jina na kuitwa Nairobi School.

Wakati huo, maisha yalikuwa magumu mno nchini Kenya kutokana na vita vya wakoloni na wapiganaji wa Mau Mau .

Vita vya mwaka wa 1952 vilimchosha na kumshawishi kuanza kupigania haki za Mau Mau. Dkt Griffin alianzisha makao ya kuwasaidia askari wa vita waliokuwa wameumia.

Baada ya miaka michache, alianzisha makao ya watoto yatima waliopoteza wazazi wao kutokana na vita vya ukoloni, ambayo baadaye aliyageuza kuwa Starehe.

Mnamo mwaka wa 1959, alianzisha Starehe Boys pamoja na Geoffrey Gatama Geturo na Joseph Gikubu. Walipata usaidizi kutoka kwa mashirika mbalimbali kama Save The Children Oxfam na mengine ili kuyakimu maisha ya watoto wa Starehe.

Wenya moyo wa kutoa wanaombwa kutuma hela zao kupitia M-pesa Paybill Number 949494, na akaunti LodwarHike.