Habari Mseto

Waliostaafu kuhesabiwa tena kuondoa wale bandia

January 23rd, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali inatarajiwa kuhesabu watu waliostaafu kutoka huduma ya umma kwa lengo la kuondoa maelfu ya wastaafu bandia ambao wanadhaniwa kupora serikali mamilioni ya fedha kila mwezi.

Kulingana na Hazina ya Kitaifa, wafanyikazi wa serikali waliostaafu 300,000 watatarajiwa kujiwasilisha katika vituo vya Huduma.

Serikali imechukua hatua hiyo kwa lengo la kudhibiti kiwango kikubwa cha pesa zinazotumiwa na serikali kila mwezi.

Pesa zinazolipwa waliostaafu zinatarajiwa kuzidi Sh100 bilioni mwaka ujao.  Idara ya Pensheni inakisia kulipa pensheni jamaa wa walioaga dunia, hali ambayo imekuzwa na mfumo wa kupata fedha za pensheni kielektroniki.

Shughuli hiyo itaanza Februari 11 ambapo waliostaafu watakuwa na mwezi mmoja kujiwasilisha vituoni humo wakiwa wamebeba vitambulisho na stakabadhi ya benki katika Kituo cha Huduma kilichoko karibu.

Hazina ya Fedha inalenga kusimamisha kuweka pesa za pensheni moja kwa moja katika akaunti za wastaafu ambao hawatafika kutambulishwa.

“Watakaokataa kufika watadhaniwa kuaga dunia na malipo kwa akaunti zao za benki yatasimamishwa,” alisema afisa wa KRA anayeelewa kuhusiana na suala hilo.