Waliosuka majonzi ya Wakenya mwaka 2018

Waliosuka majonzi ya Wakenya mwaka 2018

Na CHARLES WASONGA

MNAMO Agosti 21, 2018, Rais Uhuru Kenyatta, Kiongozi wa ODM Raila Odinga na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi walishirikiana kusukuma kupitishwa kwa Mswada wa Fedha ambao umechangia kupanda kwa bei za bidhaa muhimu nchini.

Mswada huo, ambao sasa ni sheria, ulipitishwa kwa ‘baraka’ za watatu hao licha ya pingamizi kutoka kwa baadhi ya wabunge.

Kinaya ni kwamba Bw Odinga, Spika Muturi na baadhi ya wabunge ni miongoni mwa viongozi ambao wamelaani kuongezwa kwa bei ya mafuta wiki iliyopita.

Mwishoni mwa wiki jana, Bw Muturi aliwapa changamoto wabunge alipowataka kuleta mswada wa kubatilisha sheria ya kifedha 2018 “badala ya kulalamika”.

Jumanne, Spika wa Bunge la Kitaifa Bw Justin Muturi aliipa Kamati ya Fedha siku 14 ichunguze sababu zilizochangia kupandishwa kwa bei ya mafuta na ipendekeze mabadiliko ya sheria kuipunguza.

Hii ni kufuatia malalamishi aliyopokea kutoka kwa Wakenya – Antony Manyara na John Wangai- ambao walipendekeza kuwa kipengele cha 13 cha Sheria ya Fedha, 2018 kifutiliwe mbali ili kuondoa ushuru wa VAT unaotozwa bidhaa za mafuta.

“Vile vile, ninatoa amri hii kwa mujibu wa malalamishi ambayo yamewasilishwa na Mbunge wa Matungulu Stephen Mule na ombi kutoka kwa Mbw Simba Arati (Dagoretti) na Mbunge Maalum Wilson Sossion kwamba bunge liahirishe shughuli zake za kawaida ili kujadili suala hili lenye umuhimu wa kitaifa,” Bw Muturi akasema Jumanne alasiri bunge liliporejelea vikao baada ya likizo ya mwezi mmoja.

Spika huyo aliitaka kamati hiyo ya Fedha inayoongozwa na Mwakilishi wa Homa Bay, Gladys Wanga kukusanya maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau wote husika kabla ya kuandaa ripoti itakayowasilishwa kwa kikao cha bunge lote.

Mjadala kuhusu suala hilo ulichacha bungeni huku wabunge wa mirengo yote wakielekeza lawama kwa Rais Kenyatta kutokana na mienendo yake ya kuingilia utendakazi wa asasi hiyo kwa kurejesha miswada na mapendekezo mbalimbali.

Mnamo 2018, wabunge walipopendekeza kwenye Mswada wa Fedha wa 2018 kuondolewa kwa baadhi ya ushuru kwa msingi kuwa ungelemea raia, Rais Kenyatta alikataa mapendekezo hayo na kuurudisha bungeni.

Kwenye memoranda yake kwa Bunge, Rais Kenyatta alipendekeza kurudishwa kwa ushuru huo ulivyokuwa mwanzoni pamoja na kuanzishwa kwa ushuru wa thamani (VAT) ya petroli.

Awali, Rais na Bw Odinga waliongoza mikutano ya wabunge wa mirengo yao kuwashinikiza waunge mkono kupitishwa kwa mswada huo licha ya kuwa wazi ungewatwika wananchi mzigo mzito.

Rais Kenyatta aliongoza mkutano wa kundi la wabunge wa Jubilee katika Ikulu ya Nairobi huku Bw Odinga akikutana na wabunge wa uliokuwa muungano wa Nasa katika makao makuu ya ODM.

Rais Kenyatta na Bw Odinga, waliongoza mikutano hiyo mnamo Septemba 21, 2018 asubuhi kabla ya suala hilo kujadiliwa na kupigiwa kura bungeni katika kikao cha alasiri.

Mjadala kuhusu suala hilo uliibua joto kali alasiri hiyo kati ya wandani wa Rais Kenyatta na Bw Odinga dhidi ya waliokuwa wakipinga hasa kuanzishwa kwa VAT ya mafuta.

Hatimaye kura ya sauti ilipopigwa, Spika wa Muda, Soipan Tuya alitangaza kuwa upande wa “NDIYO” ulishinda na hivyo kupitisha pendekezo la Rais Kenyatta kwenye memoranda hiyo.

Hii ni licha ya kwamba sauti ya upande wa “LA” ilikuwa na wengi zaidi.Fujo zilizuka bungeni kati ya mirengo hiyo miwili na kumlazimisha Spika Muturi kuingilia kati.

Katika uamuzi wake, Bw Muturi alimtetea Bi Tuya, ambaye ni Mbunge Mwakilishi wa Narok, akisema wakati wa kura ni wabunge 173 pekee waliokuwa ukumbini, na hivyo “mapendekezo ya Rais yamepita”.

“Takwimu zilizonaswa kwenye mitambo ya kieletroniki zinaonyesha kuwa wakati wa upigaji kura ni wabunge 173 pekee walikuwepo ukumbini. Kwa hivyo, wabunge wameshindwa kubatilisha mapendekezo ya Rais kwani kikatiba ni wabunge 233 wanaohitajika wakati wa upigaji kura,” akaeleza Bw Muturi.

Akaongeza: “Kwa hivyo, mapendekezo ya Rais yatajumuishwa kwenye Mswada wa Fedha wa 2018 kabla ya kurejeshwa kwake autie sahihi.”

Kulingana na kipengele cha 115 (1) (b) Rais ana mamlaka ya kukataa kutia saini mswada kisha kuurejesha bungeni na memoranda yenye mapendekezo kadhaa anayotaka yajumuishwe na wabunge.

Thuluthi mbili za wabunge (233) huhitajika ili kutupilia mbali mapendekezo hayo ya rais.

Rais Kenyatta aliutia sahihi mswada huo jioni hiyo hiyo, Septemba 21, 2018, na kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, bidhaa za mafuta zikaanza kutozwa VAT ya kiwango cha asilimia nane.

Serikali ililenga kukusanya Sh130 bilioni zaidi kutokana na hatua hiyo.Nayo mafuta taa yalianza kutozwa ada ya ziada ya Sh18 kwa kila lita katika kile ambacho serikali ilisema ni kuzuia mienendo ya wafanyabiashara laghai kuchanganya bidhaa hiyo na dizeli.

Sheria hii pamoja na Sheria ya Ushuru ya 2020 iliyopandisha viwango vyote vya ushuru ili kufidia mfumuko wa bei, ndiyo iliyochangia bei ya mafuta kupandishwa kwa kiwango kikubwa wiki jana.Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, petroli inauzwa kwa Sh134.7 kwa lita jijini Nairobi, dizeli Sh115.5 na mafuta taa ni Sh110.2.

Hatua hii imechangia kuongezeka kwa gharama ya maisha kwa kiwango kikubwa wakati huu ambapo raia wanaathirika na makali ya Covid-19.

Wataalamu wa uchumi wanasema wabunge wamekuwa sehemu ya matatizo ya kiuchumi yanayokumba Kenya kwa sasa.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la International Center for Policy and Conflict, Ndung’u Wainaina, wabunge hawawezi kujinasua kutokana na lawama kuhusu matatizo ya kiuchumi nchini.

“Katiba ya Kenya (2010) iliwapa wabunge mamlaka ya kuamua viwango vya ushuru, kuidhinisha bajeti na matumizi, kuweka sheria za ukopaji madeni ya kitaifa na kusimamia matumizi ya pesa zilizokusanywa kutokana na ushuru,” akasema Bw Wainaina.

You can share this post!

Wabunge lawamani kwa hali mbovu ya uchumi

Lewandowski atuzwa kiatu cha dhahabu kwa kuibuka mfungaji...