Habari Mseto

Waliotoroka makwao kufuatia fujo za kisiasa waombwa kurudi

September 17th, 2018 1 min read

Na Joseph Wangui 

Gavana wa Kaunti ya Laikipia John Mwaniki amewaomba wakazi wa eneo hilo ambao walitoroka wakati wa ghasia ambazo zilizotokea mwaka uliopita kurejea makwao.

Bw Mwaniki alisema kuwa wamefanikiwa kurejesha hali ya amani miongoni mwa jamii zinazoishi katika kaunti hiyo.

Alisema kuwa mapigano ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakitokea kati ya wakulima na jamii za kuhamahama yameathiri sana ustawi wa maendeleo katika eneo hilo.

Wakazi wengi ambao walitoroka ghasia hizo walielekea katika maeneo kama Nyahururu na Nanyuki, ambako wamekuwa wakiishi katika hali duni.

Akizungumza jana katika Shule ya Msingi ya Munyaka, Lamuria, Kaunti Ndogo ya Laikipia Mashariki, Bw Mwaniki alilalamika kwamba idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule kusoma imepungua sana.

Kampuni ya kuchapisha vitabu ya Longhorn ilitoa msaada wa vitabu wa Sh800,000 kwa ushirikiano na shirika la kijamii la Taifa Peace Ambassadors.

“Tunawaomba wazazi kuwapeleka wanao shuleni ili kuimarisha maisha yao ya usoni,” akasema.