Habari

Waliouzia NYS bidhaa hawajalipwa miaka 4 baadaye

May 22nd, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

BAADHI ya wanakandarasi halali wa Huduma ya Kitaifa ya Vijana (NYS) kufikia sasa hawajalipwa miaka minne baada ya kutoa bidhaa kwa shirika hilo.

Huku wanakandarasi haramu wakizidi kufurahia mamilioni waliyopora, wale halali waliotoa bidhaa za ujenzi walisahaulika.

Habari zilizoonekana na Taifa Leo Dijitali zilionyesha wafanyibiashara hao walitoa vifaa vya ujenzi, sehemu za magari, sare, vyakula, vitabu na kalamu na vifaa vya mawasiliano miongoni mwa vifaa vingine.

Bidhaa na huduma hizo zilitolewa wakati wa awamu ya mwanzo ya programu ya kuwawezesha vijana na mradi wa taa mitaani.

Baadhi ya wanakandarasi hao waliaga dunia, wengine waliachwa na wachumba, ilhali baadhi yao wanakabiliana na minada, kufurushwa na kufungiwa nyumba, huku wakiorodheshwa kwenye CRB kwa kulemewa kulipa madeni.

Waliozungumza na Taifa Leo Dijitali walieleza kuwa kumbukumbu yao ya NYS ni nyaraka zinazotoa ushahidi kuwa walitoa bidhaa na huduma kwa serikali.

Kulingana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Fedha za serikali Edward Ouko, NYS na wizara inayosimamia huduma hiyo haijalipa watoaji huduma na bidhaa kufikia 800 takriban Sh3 bilioni.

Kwa jumla, wanakandarasi wanadai serikali Sh11.3 bilioni katika biashara zote – halali na haramu.

Ni sakata iliyomfanya Gavana Anne Waiguru wa Kirinyaga kujiuzulu, pamoja na baadhi ya maafisa wa serikali.

Iliibuka kuwa wanakandarasi bandia walilipwa mamilioni baada ya kuwasilisha hewa NYS.

Huku hao wakiburudika, wale halali walipatwa na mshtuko wa moyo na kufa baada ya serikali kusimamisha malipo kwa wanakandarasi wote.