Habari Mseto

Waliovamia kilabu cha Simmers taabani

April 11th, 2018 1 min read

Lililokuwa lango la baa maarufu ya Simmers katika barabara ya Kenyatta Avenue jijini Nairobi. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Jumanne iliamuru kampuni mbili zilizovamia na kufunga kilabu maarufu cha Simmers, katikati ya jiji la Nairobi ziondoke mara moja.

Jaji Kossy Bor aliwaamuru wakurugenzi wa kampuni za Nilestar Holdings Limited na Green Valley Limited wafike kortini kueleza sababu walikaidi maagizo ya Jaji Lucy Gacheru ya Desemba 22 2016 kwamba wasivunje kilabu hicho, Bw Suleiman Murunga.

Bw Murunga aliyeendeleza mkahawa huo kwa miaka 21, aliambia mahakama kuu kwambe alipewa ardhi iliyojengwa kilabu hicho na Wizara ya Ardhi.

Mnamo Machi 2018, kampuni hizo zikitumia agizo lililotolewa na hakimu katika mahakama ya Milimani, zilibomoa kilabu hicho.

Jaji Bor alifahamishwa na mawakili wa Bw Murunga kwamba hakimu aliyetoa agizo kilabu hicho kibomolewe alikaidi agizo la Jaji Gacheru aliyezima ubomozi Desemba 22, 2016.

Jaji Bor alifahamishwa kwamba mawakili waliowasilisha kesi mbele ya hakimu hawakumweleza kwamba Jaji Gacheru alikuwa amesema umiliki wa ardhi iliyojengwa kilabu hicho wa Bw Murunga usivurungwe hadi kesi isikizwe na kuamuliwa.