Habari

Waliovuna enzi za Moi wasota

August 11th, 2020 3 min read

VICTOR JUMA Na BENSON MATHEKA

WANDANI wa aliyekuwa rais wa pili wa Kenya, Daniel arap Moi wanakumbwa na hali ngumu kifedha huku ikibainika kuwa mali yao ya mabilioni ya pesa inalengwa kupigwa mnada kwa kuwa wamelemewa na madeni.

Miongoni mwao ni Bw Hosea Kiplagat ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Cooperative Bank na Askofu mstaafu wa kanisa la Africa Inland Church (AIC), Silas Misoi Yego ambao hatarini kupoteza mali ya mamilioni Nairobi na Eldoret baada ya benki walizokopa kutoa ilani ya kuipiga mnada.

Wawili wao ni miongoni mwa wanasiasa, vibaraka na wafanyabiashara waliokuwa na ushawishi katika serikali ya Moi ambao wamelemewa na madeni tangu 2002 wakati aling’atuka mamlakani.

Wengine ni aliyekuwa mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo, aliyekuwa mkuu wa ujasusi Wilson Boinet, mfanyabiashara Kundan Singh wa kampuni ya Kundan Singh International na aliyekuwa waziri wa vyama vya ushirika John Cheruiyot.

Bw Kiplagat, ambaye ni mpwa wa Moi na mwenyekiti wa miaka mingi wa tawi la Baringo la chama cha Kanu, anakabiliwa na hatari ya kupoteza nyumba ya makazi mtaani Karen, Nairobi na mali ya kampuni zake ya thamani ya Sh378.61 milioni kufuatia mkopo aliochukua kutoka Bank of India.

Naye Bw Yego huenda akapoteza nyumba za makazi mtaani Kileleshwa, Nairobi baada ya kushindwa kulipa zaidi ya ShSh143 milioni alizokopa benki ya Transnational Bank.

Bw Yego alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu Rais Moi na kwa miaka mingi, aliongoza kanisa la AIC ambalo rais huyo wa pili wa Kenya alikuwa akiabudu.

Mnamo 2017, Bw Jirongo ambaye alipata umaarufu kupitia vuguvugu lililojulikana kama Youth For Kanu (YK’92) lililobuniwa kutetea Moi kubaki mamlakani miaka ya 1990s, alitangazwa kuwa amefilisika kwa kushindwa kulipa kampuni nane jumula ya Sh700 milioni.

Alipoteza mali yake nyingi baada ya kushindwa kesi kortini dhidi ya mashirika ya kifedha yaliyomdai.

Katika kesi moja, shamba la Jirongo la ukubwa wa ekari 102.7 eneo la Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia lilipigwa mnada mnamo 2017 aliposhindwa kulipa deni la Sh495 milioni alizokopa Dubai Bank ambayo kwa sasa imeporomoka.

Kampuni ya bima ya Kenya Deposit Insurance Company (KDIC) iliagiza kampuni ya madalali ya Valley Auctioneers kuuza shamba hilo kupitia mnada.

Masaibu ya Bw Kiplagat yanatokana na dhamana aliyowekea kampuni zake mbili -Eldoret Concrete Poles Limited na Timber Treatment Limited- kukopa pesa.

Kampuni ya madalali ya Garam Investments, inapanga kuuza mali yake kati ya Agosti 25 na 28.

Mbali na nyumba yake mtaani Karen, kampuni hiyo inapanga kuuza ploti 11 zinazomilikiwa na kampuni zake mbili.

Kampuni hizo zilichukua mkopo huo Mei 14, 2018 lakini zimeshindwa kulipa na kufanya benki kuuza mali aliyotumia kuzidhamini.

Kwenye ilani kwa umma, kampuni ya Garam inasema kwamba, itauza kwa mnada ekari tano za ardhi mtaani Karen Nairobi ambapo bei ya ekari moja ni Sh55 milioni kwa wastani

Hata hivyo, Bw Kiplagat amepata agizo la mahakama kusimamisha mali yake kuuzwa.

Nayo masaibu ya Askofu Yego yanatokana na pesa alizokopa Transnational Bank mnamo 2014 kupitia kampuni yake ya Siro Investments kujenga nyumba 50 mtaani Kileleshwa.

Alishindwa kulipa mkopo huo mwaka jana na kufanya benki hiyo kuagiza kampuni ya madalali ya Purple Royal Auctioneers kuuza mali yake kupitia mnada.

Askofu Yego alienda kortini kupinga mali yake kuuzwa akisema salio la deni lake ni Sh86 milioni na sio Sh143 milioni.

Lakini Jaji David Majanja aliamua kwamba Askofu Yego alikiri hakuwa amelipa deni na hangeweza kufidiwa hasara ya kesi.

Mahakama ilisema mshtakiwa alifahamu kwamba benki hiyo ingetwaa na kuuza mali yake akishindwa kulipa deni.

Jaji Majanja alitupilia mbali kesi ya Askofu Yego aliyotaka benki izuiwe kuuza mali yake.

Kwa upande mwingine, mnamo 2015, Bw Cheruiyot alikamatwa na kutupwa jela miezi sita kwa kushinda kulipa deni la Sh2.3 milioni kwa muda wa miaka 20.

Waziri huyo wa zamani alikuwa ameagizwa kumlipa mfanyabiashara Antony Lang’o pesa hizo kwa kumuuzia kofia za chama cha Kanu mnamo 1994.

Kampuni ya ujenzi ya Kundan Singh, ambayo ilivuma katika enzi za utawala ya Moi, ilikumbwa na kesi mahakamani ilipofilisika miaka ya hivi majuzi.

Kando na mvutano kuhusu agizo kwamba kampuni hiyo iwekwe chini ya mrasimu, wamiliki wake walidaiwa kukwepa kulipa ushuru wa takriban Sh226 milioni kati ya mwaka wa 2010 na 2015.