Habari

Waliowika KCSE wafichua siri za ufanisi

December 19th, 2019 2 min read

Na WANDISHI WETU

MWANAFUNZI aliyefanya vyema zaidi katika Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) wa 2019, Jumatano, alikuwa akichapa kazi kwenye shamba la Babu yake katika eneo la Mumias, Kaunti ya Kakamega bila kujua kwamba angekuwa nyota jioni.

Buluma Wabuko Tony alipata Gredi ya A kwa alama 87.1 na kuibuka kidedea baada ya kuwashinda watahiniwa wote 699,745 waliofanya mtihani huo kati ya Novemba 4 na Novemba 27.

Familia yake ilitarajia kwamba angefanya vyema lakini hawakudhani kwamba angeibuka bora zaidi nchini.

Wakiwa shambani, mjomba yake Collins Lutta alimtania kwamba angependa kumwona kwenye runinga au gazeti baada ya matokeo ya KCSE kutangazwa.

“Nilijua kwamba angefanya vyema. Hata tulipokuwa shambani nilimtania kwamba ningetaka kumwona akihojiwa na wanahabari. Lakini sikutarajia kwamba yeye ndiye angeibuka kidedea nchini. Ameleta mwangaza katika kijiji chetu,” akasema Bw Lutta.

Tony anaazimia ya kuwa daktari. Kwa sasa yuko nyumbani kwa Babu yake kijijini Emakhwale, Mumias Mashariki, ambapo alienda kwa ajili ya sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Tony, 15, amekuwa akifanya vyema shuleni tangu alipokuwa shule ya msingi.Katika mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) wa 2015, Tony alipata 433 kati ya 500 katika shule ya msingi ya St Aquinnas iliyoko katika eneo la Njoro, Kaunti ya Nakuru.

“Nimekuwa nikitia bidii masomoni na nilifahamu kwamba ningefanya vyema katika mtihani wa KCSE. Lakini sikutarajia kuibuka mwanafunzi bora nchini. Matokeo yalinishtua mimi pamoja na familia yangu,” anasema.

Anasema mafanikio yake yalitokana na bidii masomoni, nidhamu na kumcha Mungu. Mwanafunzi aliyeibuka nafasi ya tatu nchini Aboge David Johnson Odhiambo, pia alikutana na Taifa Leo katika mtaa wa mabanda wa Nyalenda, Kisumu.

Aboge alipata alama 87.08 na alikuwa akisomea Shule ya Upili ya Kapsabet.Ijapokuwa hakufanikiwa kujiunga na Shule ya Upili ya Alliance alivyotamani, hilo halikumzuia kutia bidii masomoni na kuwa mwenye nidhamu hadi kuibuka wa tatu bora kitaifa.

Sasa anaazimia kujiunga na Chuo Kikuu cha Harvard kusomea udaktari.Kwingineko, shamrashamra zilikuwa zimenoga katika Wadi ya Orolwo Kodich ward , Pokot Kaskazini baada ya Mourine Chepengat Longal, 17, aliyekuwa akisomea katika shule ya Upili ya Wasichana ya Alliance kuzoa alama 86.97 katika mtihani wa KCSE ambao matokeo yake yalitangazwa Jumatano.

Chepengat aliibuka katika nafasi ya saba kote nchini.Aliongoza katika Kaunti ya Pokot Magharibi kwenye mtihani wa KCPE aliofanyia katika shule ya Town View Academy.

Miaka minne tangu kuhitimu kutoka katika shule ya Town view Academy, hakuna mwanafunzi ambaye amevunja rekodi yake.

Mwanafunzi aliyeibuka kidedea katika Kaunti ya Homa Bay Anthony Owuor Ochieng’ alikuwa kanisani kabla ya kupokea habari kwamba aliibuka katika nafasi ya nne nchini katika mtihani wa KCSE.Anthony, maarufu “Harvard” (Chuo Kikuu cha Harvard), aliibuka nafasi ya kwanza katika shule ya upili ya Maseno, Kaunti ya Kisumu, baada ya kupata alama 87.

Anthony anaishi katika kijiji cha Olodo na alisomea katika Shule ya Msingi ya Asego mjini Homa Bay ambapo alipata alama 425 kati ya 500.

Ripoti za Shaban Makokha, Oscar Kakai, George Odiwuor, Donna Atola Na Angeline Ochieng