Waliozua fujo watatiwa adabu au ni vitisho baridi tulivyozoeshwa?

Waliozua fujo watatiwa adabu au ni vitisho baridi tulivyozoeshwa?

Na WANDERI KAMAU

TUME ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imewaagiza wabunge 10 kufika mbele yake hapo kesho, kufuatia ghasia zilizotokea kwenye chaguzi ndogo zilizofanyika Alhamisi katika sehemu kadhaa nchini.

Wanasiasa hao ni Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Homa Bay, Bi Gladys Wanga, Millicent Omanga (Seneta Maalum), Aisha Jumwa (Malindi), Feisal Bader (Msambweni), John Waluke (Sirisia), Fred Kapondi (Mt Elgon), Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Charles Were (Kasipul), Chris Wamalwa (Kiminini) na Seneta Cleophas Malala (Kakamega).

Wabunge hao wanatuhumiwa kuchochea ghasia zilizoshuhudiwa kwenye chaguzi ndogo zilizofanyika katika maeneobunge ya Matungu na Kabuchai katika kaunti za Kakamega na Bungoma mtawalia.

Ghasia pia zilitokea katika wadi za London (Nakuru) na Kiamokama (Kisii).

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, mwenyekiti wa tume hiyo, Dkt Samuel Kobia alisema kuwa mbali na kuchunguza jinsi wanasiasa hao walivyoshiriki kwenye ghasia hizo, wanatathmini hatua zitakazochukuliwa kuhakikisha wamezuiwa kuhudumu ama kuwania nafasi za uongozi.

“Tumeiandikia barua Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuhakikisha imepata kibali kutoka kwa Idara ya Mahakama kuanza mchakato wa kuwaondoa mamlakani viongozi ambao wanakiuka Kipengele cha Sita cha Katiba kuhusu uongozi,” akasema Dkt Kobia.

Alisema kuwa sawa na vile watumishi wa umma wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi wanavyoagizwa kuondoka nyadhifani, mkondo uo huo ndio unaopaswa kufuatwa kuwakabili viongozi wanaokumbwa na madai ya uchochezi.

Kauli hiyo inajiri baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, kuonya kuwa viongozi ambao walihusika kwenye ghasia hizo watanyang’anywa bunduki zao.

“Nimeiagiza Bodi ya Kutoa Leseni za Bunduki (FLCB) kusimamisha leseni za viongozi wote waliohusishwa na ghasia zilizotokea Alhamisi. Ni wazi kuwa kulingana na sheria, huwezi kuruhusiwa kuendelea kumiliki bunduki kama umehusika katika vitendo kama hivyo,” akasema Dkt Matiang’i, alipohutubu kwenye hoteli moja jijini Nairobi.

Alisema ameshauriwa na Mwanasheria MKuu kwenda mahakamani kuhakikisha kuwa kanuni za Kipengele cha Sita cha Katiba zinazingatiwa, ambapo viongozi wote wanaokiuka sheria watazuiwa kuwania nafasi yoyote ya uongozi.

Alikosoa mchakato wa kisheria ambapo viongozi wanaoshtakiwa kwa uchochezi huwa wanaachiliwa kwa dhamana za chini kama Sh10,000 huku kesi zao zikijikokota kwa miaka.

Mnamo Ijumaa, wabunge wanne ambao ni washirika wa Naibu Rais, Dkt William Ruto walishtakiwa katika mahakama moja ya Bungoma kwa tuhuma za kuzua ghasia katika eneobunge la Kabuchai.

Wabunge Didmus Barasa (Kimilili), Nelson Koech (Belgut), Wilson Kogo (Chesumei) na Seneta Samson Cherargei (Nandi) walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Stephen Mogute, ambapo walikana mashtaka hayo.

Waliachiliwa kwa dhamana za Sh50,000 ama Sh100,000 pesa taslimu kila mmoja. Kesi yao imepangiwa kusikilizwa Aprili 6.

Matukio hayo yanajiri huku wadau mbalimbali wakieleza wasiwasi wao kutokana na mwelekeo wa kisiasa nchini.

Mwelekeo huo umeelezwa kuchangiwa na siasa za ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) na uchaguzi mkuu wa 2022.

Hapo jana, Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) ilieleza hofu kuhusu usalama wa wafanyakazi wake, baada ya mmoja wa maafisa wake kupigwa kofi na aliyekuwa Waziri wa Michezo, Rashid Echesa katika eneobunge la Matungu, huku mwingine akitolewa kwa nguvu kutoka kituo cha kupigia kura na watu waliobeba silaha katika eneo lilo hilo.

Polisi washamkamata Bw Echesa kutokana na kisa hicho.

You can share this post!

Kenya Cup: KCB yalemea Quins kwa jasho Kabras iking’aria...

ODM: Raila anachezwa