Michezo

Walishwa kadi nyekundu kwa kuvunja sheria mbio za Birmingham

March 4th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KWA mara kwanza katika historia ya Riadha za Dunia za Ukumbini wakimbiaji wote katika mbio za mchujo mmoja walionyeshwa kadi nyekundu kwa kuvunja sheria mjini Birmingham, Uingereza, Ijumaa.

Mshindi wa medali ya fedha mwaka 2016, Abdelalelah Haroun alikuwa wa kwanza kuaga mashindano alipolishwa kadi nyekundu kwa kuanza kutimka kabla ya mlio wa bastola ya kuanzisha mbio kulia.

Washiriki wengine katika mchujo huo wa tatu – Steven Gayle (Jamaica), Austris Karpinskis (Latvia), Alonzo Russell (Bahrain) na Bralon Taplin (Grenada) – wote walianza vyema mbio hizo za mzunguko mmoja na hata kuzikamilisha.

Hata hivyo, wanne hao walipatikana na hatia ya kuvunja sheria za kubadilisha laini na kuondolewa mashindanoni.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Riadha duniani (IAAF), hii ni mara ya kwanza kabisa Riadha za Dunia za Ukumbini zimeshuhudia wakimbiaji wa mchujo mmoja wakiondolewa mashindanoni.

Taplin ni mmoja wa wakimbiaji waliokuwa wamepigiwa upatu kuzoa medali ya dhahabu katika makala haya ya 17. Michujo ya kwanza, pili, nne na sita haikuwa na visa hivi. Nerry Brenes kutoka Costa Rica, ambaye alishiriki mchujo wa tano, pia hakuwa na bahati alipovunja sheria za mashindano.

Kenya haikuwakilishwa katika mbio za mita 400 za ukumbini mwaka huu wa 2018. Boniface Mweresa alimaliza makala ya mwaka 2016 katika nafasi ya tano nchini Marekani.